Mbatia aibua hoja ya Katiba Mpya

28Apr 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mbatia aibua hoja ya Katiba Mpya

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amesema ipo haja ya kuwapo kwa tume huru ya maridhiano ambayo itazaa upatikanaji wa Katiba mpya, itakayotokana na wananchi.

Amesema mchakato wa upatikanaji Katiba mpya ulioanzishwa mwaka 2013 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na kupatikana Katiba iliyopendekezwa bungeni, haukupatikana kwa mfumo wa wananchi.

Mbatia aliyasema hayo jana jijii Dar es Salaam, katika mahojiano maalum na Nipashe, kuhusu masuala mbalimbali yakiwamo ya hali ya kisiasa nchini.

Alisema ili kufikia mwafaka wa kitaifa iliyo na umoja, inahitajika suluhu ya kisiasa kutoka kwa wananchi kupitia meza ya majadiliano.

“Zao la Katiba lilianzishwa na rais, si sawa. Pamoja na kumpongeza Kikwete kuanzisha mchakato ule, udhaifu wa mfumo wetu ulifanya rais aanzishe mchakato huo, bado ilitakiwa mchakato uanzishwe na wananchi, sababu ni wa wananchi.

“Katiba ni mama, Bunge, Mahakama, serikali ni mtoto, na rais yupo ndani ya Katiba, utaona upatikanaji wake haukuwa wa wananchi,” alisema Mbatia.

Kuhusu rasimu ya Jaji Joseph Warioba, alisema inaweza kuwa ni Katiba itakayotokana na wananchi, kutokana na maandalizi yake kuhusisha maoni ya wananchi.

“Katiba hii tuliyonayo sasa ya mwaka 1977, pamoja na kufanyiwa marekebisho kadhaa, bado inaminya demokrasia na uwanja usio sawa wa kisiasa.

“Katiba inatoa haki ya kufanya siasa kwa vyama vya siasa vilivyosajiliwa, lakini wakati huohuo inapoka uhuru na haki hiyo, kwamba marufuku mikutano ya kisiasa kwa vyama,” alifafanua Mbatia.

Aliongeza kwamba Katiba iliyopo sasa inatoa madaraka makubwa kwa rais na kuwateua viongozi mbalimbali ikiwamo wakuu wa mikoa, wilaya na hata wakurugenzi.

“Tume ya mabadiliko ya Katiba ni mawazo kutoka kwa wananchi, ikizingatiwa tunu za taifa, uzalendo, uadilifu, umoja na uwajibikaji, likaja bunge likagawanyika katika misingi ya kiitikadi na upande mmoja ulitengeneza Katiba iliyopendekezwa.”

“Katiba iliyopo ya mwaka 1977, bado ni ya mfumo wa chama kimoja, Ibara ya 10 inatoa haki ya kuruhusu mikutano ya kisiasa lakini ina upungufu mkubwa,” alisisitiza Mbatia.

Kadhalika, Mbatia alisema kuwapo kwa vyama ambavyo havina ushindani kunatokana na Katiba ambayo haitoi uhuru wa kidemokrasia kwa usawa kutokana na baadhi ya vifungu.

Alibainisha kwamba kukubalika mfumo wa vyama vingi mwaka 2010 ilikuwa ni kwa asilimia 48 hadi 50 na hivi sasa vyama vingi vinahitajika kwa asilimia zaidi ya 80.

“Maendeleo ni watu, kurudishwa nyuma kwa vyama vya siasa katika uwanja huru wa kidemokrasia, kutokana na kuitumia Katiba hii hii, kwamba dola izuie mikutano kumerudisha nyuma juhudi za kwenda mbele.

“Vyama vya siasa sasa vinazungumzia udini, ukabila, kutokana na kukosa hoja imara za kisiasa, fikra zimerudi nyuma hakuna kufikiri shughuli za msingi katika kulijenga taifa.”

Akizungumzia serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, alisema ikitoa fursa ya uhuru wa vyombo vya habari, haki na demokrasia kutaifanya nchi kusonga mbele.

 

“Hivi sasa vyombo vya habari ndio kila kitu. Media ni bidhaa ghali zaidi duniani naweza kusema ni taarifa, sababu inatoa taarifa za mahali popote na taarifa ni maendeleo, unapominya uhuru inaathiri kila kitu.”

Alisema pamoja na hotuba za Rais Samia kugusia masuala mbalimbali ambayo yanarudisha demokrasia nchini, akumbuke suala la jinsia kwenye nyadhifa tofauti za uongozi.

“Kwa namna gani rais anashawishi wanawake na wasichana katika uongozi, iwe rejea kwa bara la Afrika, sauti za uhuru wa kifikra zikasikika.”

*Usikose kufuatilia mahojiano kwa upana kesho