Mbatia: Utashi wa kisiasa muhimu kwa maendeleo

29Apr 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mbatia: Utashi wa kisiasa muhimu kwa maendeleo

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amesema ili kurejesha nchi katika demokrasia, haki na uhuru wa kujieleza, kunahitajika utashi wa kisiasa.

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, akifanya mahojiano na mwandishi wa makala hii Christina Mwakangale.

Amesema vyama vya upinzani havifanyi vizuri katika nyanja ya kisiasa hali inayosababisha kuwapo kwa hoja dhaifu ambazo hazina mustakabali mzuri kwa taifa.

Katika mahojiano maalumu na Nipashe, Mbatia  amezungumzia masuala mbalimbali, ikiwamo hali ya kisiasa, demokrasia, haki na uhuru wa kujieleza.

Swali: Unaonaje hali ya kisiasa hivi sasa nchini?

Jibu: Ninaweza kusema hivi, hali ya kisiasa nchini ipo kwa namna hii, ila kwanza umma ufahamu maana ya siasa. Siasa kwa wanaoamini kwamba Mungu yupo, kwenye mambo ya uumbaji, ni kwamba kila binadamu ana fikra tofauti na mwenzake na ni haki ya msingi. Unaweza ukakubali kwamba ukifikiri sana ikafikia hatua kwamba imani za dini, sayansi, siasa vimekuwa kitu kimoja.

Mwaka 1633 Kanisa Katoliki lilimpinga mtu aliyesema dunia inazunguka jua, huyu alikuwa Galileo Galilei, ambaye alihukumiwa kufungwa, kwa kauli hii. Baadaye mwaka 1992, Papa Yohane Paulo II, aliomba radhi kuwa hiyo hukumu haikuwa sahihi.

Kwa kuwa sisi ni binadamu na tuna mawazo tofauti kila mmoja atasema twende Kaskazini, Kusini mwingine Magharibi, Mashariki, ili kuafikiana tufanye lipi lazima fikra ziwe pamoja kwa kukubaliana twende upande huu, ili kuifanya dunia iwe sehemu salama ya kuishi.

Katika muktadha huo, siasa ndio huileta jamii pamoja na kukubaliana itikadi yetu, imani iwe namna gani ili tuishi. Kila mmoja anaonesha ushawishi wa itikadi yake utakuwaje, ili kutofutisha chama kimoja na kingine.

Swali: Nini umuhimu wa vyama vya upinzani kisiasa?

Jibu: Vyama vya siasa vipo kwa ajili ya kushindanisha hoja. Na ili kuifanya Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kuishi kuna utaratibu wa kikatiba. Utaratibu huu ili ufanyike kuna Katiba iliyoweka misingi. Katiba ya sasa ya mwaka 1977, inatoa nafasi, haki ya chama cha siasa kufanya kazi kwa misingi iliyowekwa.

Kuna kanuni, sheria, ili kujumuika pamoja, kufanya mikutano ya hadhara kwa vyama, ni haki ya kimsingi.

 

Pamoja na mabadiliko yote yaliyofanyika katika Katiba hii bado ni ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, itikadi imeandikwa kwenye Katiba kuwa ni ya ujamaa na kujitegemea.

Ibara ya 10 inasema CCM itakuwa ni chama pekee, ikafutwa. Ilivyofutwa na nyingine zikabaki kama ilivyo, hii ikatupa shida, japo ibara moja inatoa haki, nyingine inafinyanga hiyo haki.

Wanazuoni walisema Katiba itokane na umma. Kwa hiyo Katiba hii inatoa haki na wakati huohuo ina upungufu mwingi.

Mwaka 1991 tuliweka msukumo wa kuandikwa kwa Katiba Mpya na kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Tulikutana kwa siku mbili na kuanzisha Kamati ya Jaji Nyalali, kuuliza Watanzania inatakiwa Katiba ipi. Lakini waliokuwa madarakani hawakutaka kutekeleza yaliyokuwa kwenye Tume, zaidi walibeba pendekezo la kuwa na vyama vingi.

Mfumo mwingine ukabaki kama ulivyo, vyama vingi vipo lakini kwa hisani ya chama kimoja.

Chama cha Mapinduzi kilisajiliwa moja kwa moja bila utaratibu kwa kuomba kama chama cha siasa, ndio maana kuna hoja nyingi za msingi kuwa CCM sio chama cha siasa bali ni chama dola kwa mujibu wa sheria.

Baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa ilitakiwa vyama vianze kusajiliwa. Sheria mpya ikasema CCM ilisajiliwa moja kwa moja bila utaratibu wa kupata wanachama 200 katika mikoa ikiwamo Zanzibar.

Swali: Kwa nini kuna ukimya wa kisiasa kwa vyama vya siasa, hasa upinzani?

Jibu: Hamu kubwa kwa wananchi ni kuwa na kitu kinachoitwa utashi wa kisiasa. Mambo yanayohusu siasa kuzingatiwa kwa upana wake.

Vyama vinatakiwa kufanya majukumu yake kwa kushindana, lakini vikisimamiwa na chama kilichopo madarakani, chama dola, ambacho tangu uhuru ni kilekile, tunasema ni chama dola sababu kinachukua muundo wa serikali. Vyombo vyote ikiwamo vya ulinzi na usalama vinaripotiwa kwake kwa chama kilichopo madarakani.

Kwenye hali ya namna hiyo hivi sasa ushindani wa fikra, hamasa za maendeleo endelevu kunadumazwa na siasa kwa kutokuwapo uwanja sawa wa siasa.

Utaratibu ukiwa si hai, unadumaza siasa. Sasa hivi kuna kasi ya kutaka mfumo wa vyama hivi ni hoja kielelezo. Ukiangalia mtawanyo wa umri wa watu wazima, wenye umri wa miaka 16 hadi 54 ni asilimia 85 ya Watanzania wote. Hawa wote wamezaliwa baada ya Muungano.

Kuna hoja zinazoibuka kutoka kwa wananchi ambazo zinakosa uendelevu, ni kiburi cha wanasiasa kujiona bora kuliko mwingine. Sisi wanasiasa tunaoleta kiburi cha kisiasa kwenye jamii.

Swali: NCCR-Mageuzi inaendeleaje katika ulingo wa kisiasa kwa kutofanya mikutano?

Jibu: Kwenye Katiba vyama vinaruhusiwa mikutano, ninaweza kusema kipindi hiki serikali haikuwa rafiki wa demokrasia, Tanzania tunaihitaji zaidi dunia, kuliko sisi tunavyoihitaji.

Huwezi ukazungumzia jambo lolote kabla ya kuzungumzia haya manne, utawala wa sheria, utawala bora, demokrasia na haki za binadamu. Ukitaka kuzungumza jambo lolote ikawa hakuna nafasi. Ustawi wa mwanadamu kulinda uhai wake, kifikra, mawazo mbadala.

Maendeleo ni watu si vitu. Ubunifu wa Mwalimu Nyerere kuunganisha watu kuzungumza lugha moja ya Kiswahili, ni maendeleo.

Swali: Vyama vya siasa vimeathirika vipi?

Jibu: Sio tu imeathiri vyama vya siasa, imerudisha nyuma Tanzania kwenye ujima. Hii imeturudisha Watanzania kuzungumza hoja zisizo na msingi kwenye maofisi, vyama vyetu hasa kuhusu ukabila, vyama tumerudi kuzungumzia udini, maeneo, kila mtu kumtilia shaka mwenzake.

Marufuku hii imeathiri na kudhoofisha upinzani na hata CCM yenyewe. Itachukua miaka takribani 10, kurudi tena.

Tanzania imeshika nafasi ya 153 kati 156 ya watu wake kuwa na furaha. Hii ni kurudi nyuma kwa maendeleo ya kifikra, demokrasia. Uhuru wa taarifa, kushirikishana ni muhimu sana.

Swali: Unazungumziaje serikali awamu ya sita?

Jibu: Tunahitaji meza ya majadiliano tukijadiliana katika meza ya mazungumzo, tutajua tufanye nini. Ukiniuliza kwenye hiyo meza cha kwanza tutengeneze tume ya majadiliano kuleta suluhu na maridhiano kwa mambo ya msingi.

Hapo itapatikana, Tume Huru ya Uchaguzi, Katiba Mpya, meza ya majadiliano itazaa maafikiano. Rais atakuwa amejijengea heshima kwa kuundwa kwa tume ya suluhu, na kisha twende kwenye Katiba.

Mimi nitasema kuhusu Katiba, nitasema twende na ya Jaji Warioba, au tuamue kufanya mabadiliko katika Katiba hii ya mwaka 1977 iliyopo, tutakubaliana.

Ili kuzaa mwafaka wa kitaifa tunaweza kujifunza kutoka hata Zanzibar, aliifanya Maalim Seif (marehemu), Kenya walifanya na tulishiriki katika meza ya mazungumzo.

Mwaka 2013, watu 96 akiwamo rais, maspika, makamu wa rais, viongozi wa dini na serilaki, tulikaa kwa siku chache tulimaliza hali ambayo kipindi hicho ilihatarisha usalama na amani.

Ili mama (Rais Samia) aweze kufanikiwa utashi kisiasa uwepo.

Swali: Nini kifanyike kufikia Tanzania ya maendeleo na demokrasia?

Jibu: Katiba inazungumzia yote, Tume ya Uchaguzi ipo kwenye Katiba, Msajili wa vyama yumo katika Katiba, ukiwa na Katiba Mpya kila kitu kitazaliwa kipya.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa itafanya kazi yake. Mfano tangu vyama vilipopigwa marufuku hakuna hata chama kimoja kilichosajiliwa, uhuru wa mahakama vyote vitapatikana kupitia Katiba.

Swali: Ukikutana na Rais Samia ukiwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, una ajenda gani za kumpa?

Jibu: Hivi karibuni Kamati Kuu ya chama ilipokutana siku mbili, tulizungumza mambo mengi na Machi 29, mwaka huu, tulimuandikia barua Rais Samia, kumpongeza, tulimwambia tupo tayari kufanya naye kazi katika kustawisha mifumo yenye kujali utu wa mwanadamu.

Alitujibu April 14, mwaka huu, na tunasubiri akituita tuzungumze masuala ya msingi, kama chama upande wetu, Katiba, lakini kuu la msingi ni kuhusu mifumo imara ambayo huzaa haki na amani.

Swali: Vyama vya upinzani ni kundi lenye tafsiri gani kwenye jamii?

 

Jibu: Mfano kuna wabunge ambao wamekataliwa na vyama vyao, lakini mhimili wa Bunge unasema hapana tunawatambua hawa ni wabunge. Kuna fujo zinatokea kwenye siasa na kupunguza au kuondoa imani.

Fujo kwenye vyama inatokana na imani kushuka na kutoaminiana. Hakuna utaratibu wa kutekelezeka kama ilivyowekwa.