Mbeya, Iringa zatajwa utapiamlo

11Jul 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mbeya, Iringa zatajwa utapiamlo

​​​​​​​MIKOA ya Mbeya, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa na Ruvuma, imetajwa kuwa kinara wa utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano licha ya mikoa hiyo kufanya vizuri katika uzalishaji wa mazao ya chakula.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Andrea Pembe, aliyabainisha hayo juzi mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kutoa matokeo ya utafiti uliofanywa katika mikoa mbalimbali nchini.

Alisema lengo la utafiti huo uliofanyika Machi mwaka huu na kushirikisha wananchi ni kuangazia mila, desturi na tamaduni zinazoweza kuchangia utapiamlo katika mikoa hiyo.

Alisema utafiti huo ulishirikisha MUHAS, Shule ya Afya ya Jamii, Chuo Kikuu cha De Montfort cha Uingereza na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kwa ufadhili wa Global Challenge Research Foundation.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za 2016, asilimia 31.5 ya watoto walio chini ya miaka mitano, wana utapiamlo kutoka asilimia 48 kwa mwaka 1999.

Alisema kiwango hicho bado ni cha juu licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali na kwamba wanaamini kuwapo kwa chakula cha kutosha hakuwezi kuwa sababu ya kupata utapiamlo kwa watoto hao ndiyo sababu wakaamua kuchunguza mila na desturi zinazochangia hali hiyo.

"Ingawa serikali ina juhudi inazofanya za kuongeza uzalishaji wa chakula, kuweka mikakati ya huduma bora za jamii wakiwamo watoto chini ya miaka mitano, mpango mkakati wa kupunguza utapiamlo na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mbinu za utapiamlo lakini bado kiwango cha utapiamlo kipo juu kwa mikoa yenye chakula," alisema Profesa Pembe.

Alisema wanafikiri kunaweza kuwa na sababu nyingine inayofanya kuwapo kwa utapiamlo katika mikoa hiyo na ndiyo maana wanajadili namna ya kupata sababu za kuwapo kwa hali hiyo.

Alisema wamekutana waliofanya utafiti na wadau walioshirikishwa kwa lengo la kuchambua ripoti kama inaakisi uhalisia.

Alisema baada ya hapo watakwenda ndani ya jamii kufanya uchunguzi wa sababu za watoto kupata utapiamlo hasa kwa kuzingatia kuwa wana vyakula vya kutosha.

"Siyo tu upatikanaji wa chakula pekee ndiyo sababu ya utapiamlo, ni utuamiaji wa chakula au ugawaji na mila na desturi za Watanzania ndiyo unasababishwa utapiamlo na ndiyo maana tumefanya utafiti huu," alisema Profesa Pembe.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Wizara ya Afya, Dk. Ama Kasangala, alisema waliamua kufanya utafiti huo ili kubaini sababu za kuwapo kwa utapiamlo katika mikoa hiyo licha ya kuwa ina chakula cha kutosha.

Alisema lengo ni kupata chanzo halisi ili kuandaa sera za mwongozo wa kutoa elimu kwa umma namna ya kudhibiti utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano nchini.

Habari Kubwa