Mbinu kukwepa imani za kishirikina yatajwa 

18Mar 2019
Jumbe Ismaily
IKUNGI
Nipashe
Mbinu kukwepa imani za kishirikina yatajwa 

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, amewataka wananchi wilayani mwake kuitumia fursa za kuichumi zilizoko kwenye maeneo yao, kuongeza vipato vyao, akiamini mtu mwenye uchumi mzuri hawezi kuwaza kulogwa.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu, wakati wa kukabidhi kisima kwa Kitongoji cha Taru, kilichoko kata ya Mang’onyi, wilayani Ikungi mwishoni mwa wiki, Nchimbi alisema ikiwa kipato cha wananchi kitaongezeka, imani za kishirikina zitatoweka katika jamii.

“Sasa ndugu, kipato kizuri kikiwapo, maneno maneno yanatoweka, uchumi ukikua, hauwazi tena kulogwa, ndiyo uzuri wa uchumi," Nchimbi alieleza katika hotuba yake hiyo.

Alisema mkoa wake bado unakabiliwa na changamoto ya baadhi ya wakazi wake kuamini dhana potofu kuwa mwili wa mtu mwenye ualbino ni utajiri, akibainisha kuwa baadhi ya wachimbaji wa madini wanaotaka njia za mkato za kutajirika hutumia viungo vya watu wenye ualbino kuendesha shughuli zao za uchimbaji.

"Yaani unamkuta mtu anahangaika eti achukue kiungo, kiungo gani? Huyo mwenyewe mwenye mwili hajawa tajiri, wewe ukate kiungo tu," alisema.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja Mkuu Mradi wa Shanta Singida, Philbert Rweyemamu, alisema kisima hicho kimegharimu Sh. milioni 51.5 zilizotumika katika utafiti, uchimbaji na utayarishaji kisima, pampu, kipimo cha usalama wa maji, ujenzi wa miundombinu na mfumo wa umemeja.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mohamedi Ramadhani, aliipongeza Kampuni ya Shanta kwa utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kulinda miundombinu yake yote.

Habari Kubwa