Mbinu kumaliza uhaba mafuta ya kula zatajwa

24Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mbinu kumaliza uhaba mafuta ya kula zatajwa

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo ina mpango wa kuongeza nguvu katika uzalishaji wa alizeti ili kuhakikisha kuna mafuta ya kula ya kutosha yanayozalishwa nchini na hivyo kupunguza utegemezi wa mafuta hayo kutoka nje.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo sasa, uzalishaji wa ndani unakidhi asilimia 43 na hivyo nchi inazalisha tani 270,000 za mafuta ya kula kila mwaka na huagiza nyingine tani 600,000 kufidia pengo lililopo ndani.

Prof. Mkenda aliyasema juzi alipozuru kwenye kiwanda cha kusindika mafuta ya kula ya alizeti cha Pyxus Agriculture Tanzania cha jijini Dodoma.

Alisema pamoja na kuongeza nguvu kuhakikisha mafuta ya kula yanapatikana nchini kwa kiasi kinachotakiwa, serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji na pia wakulima wadogo kwa kuwapa nafasi ya kusafirisha bidhaa zao nje.

Prof. Mkenda alisema kwamba anafahamu kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanasababishwa na kukwama kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta nchini, hivyo serikali itapitia upya sheria na kanuni ili kuondoa mkwamo na kuwezesha uzalishaji wa ndani kukua zaidi.

Waziri Mkenda alisisitiza kuwa hakuna mageuzi ya kiuchumi yanayoweza kutokea bila kuwa na mapinduzi kwenye kilimo.

"Tukiongeza tija kwenye kilimo, bei za bidhaa kama chakula itapungua, mageuzi kwenye kilimo yatasaidia sana kukuza viwanda hapa nchini," alisema Prof. Mkenda.

Waziri huyo alisema serikaĺi itahakikisha mbegu za kutosha za alizeti zinapatikana, akiagiza kuangaliwa kwa mfumo wa kilimo cha mkataba kwa kuboresha mfumo wake.

"Tabia ya watu kuingia mkataba lakini wakati wa kuvuna wanampa mtu mwingine haipendezi, lazima wakulima waheshimu mikataba.” alionya Prof. Mkenda.

Waziri huyo aliongeza kuwa ataitisha mkutano wa wataalamu ili kuangalia upya sera na taratibu zinazotumika katika uzalishaji wa alizeti nchini.

Hata hivyo alikiri kwamba mahitaji ya mafuta ya kula nchini yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa corona ambao umesababisha mwenendo usiokuwa wa afya kwa biashara ya kimataifa ikiwamo ya mafuta ya kula.

Waziri aliwaambia wamiliki wa Kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania kwamba serikali haijazuia upelekaji wa mafuta ya kula nje na kwamba kuchelewa kwa maofisa wa serikali kutoa vibali kunaathiri wakulima wadogo nchini ambao wanategemea kiwanda kama hicho kupata soko la uhakika.

“Kiwanda hicho kimepata soko katika Jumuiya ya Ulaya kupeleka mafuta yaliyosafishwa mara mbili (Double Refined). Tuna uwezo wa kuilisha nchi yetu na mafuta tunayozalisha wenyewe na kuuza mengine nje,” alisema.

“Wataalam wanasema kama wakulima wakibadilika na kufanya kilimo biashara chenye matumizi ya zana za kisasa na mbegu bora za kisasa, wataweza kuzalisha tani 10 za alizeti kwa hekta.

“Kwa sasa, wakulima nchini wanazalisha chini ya tani moja kwa hekta," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania, Malcolm McGrath, alisema kiwanda chake kwa sasa kinazalisha tani 20,000 kwa mwaka lakini kina uwezo wa kuzalisha mara sita zaidi ya hapo.

Mkurugenzi huyo alisema tayari wamekuwa na mawasiliano na wakulima wadogo, wa kati na wakubwa wa alizeti kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro, Manyara, Singida, Tabora na Kigoma lakini kuna kikwazo kikubwa cha ughali wa malighafi, hivyo kufanya bidhaa yao kuwa ghali kulinganisha na nchi nyingine zinazopeleka mafuta katika soko la Ulaya.

Mwenyekiiti wa Shirikisho la Wachakataji Alizeti Mkoa wa Dodoma, Ringo Iringo, alisema kuna kikwazo katika masuala ya tozo mbalimbali na kodi ya ongezeko la thamani kwa teknolojia inayoingizwa nchini.

Habari Kubwa