Mbinu mpya uporaji fedha Dar hizi hapa

06Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mbinu mpya uporaji fedha Dar hizi hapa
  • *Polisi yatoa angalizo, wenye benki wafunguka

WAKATI Jeshi la Polisi likiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukomesha vitendo vya uporaji wa fedha vilivyoibuka kwa kasi jijini Dar es Salaam katika siku za hivi karibuni, imebainika kuwa sasa zipo mbinu mpya zilizobuniwa na waporaji kukamilisha uovu wao.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kuhusisha mahojiano na watu mbalimbali waliowahi kukumbwa na kadhia hiyo, polisi na wadau wa masuala ya fedha jijini humo, umebaini kuwa njia hizo mpya ni pamoja na ile ya waporaji wanaotumia pikipiki maarufu kama bodaboda kuifukuzia gari ya mtu aliyebeba fedha kwa kudai kuwa imesababisha ajali sehemu.

Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini njia nyingine mpya kuwa ni ile ya waporaji kujifanya wasamaria wema kwa kuifuata gari wanayojua kuwa ndani yake kuna fedha na kumpa dereva ishara inayoonyesha kuwa gari yake ina tatizo kabla ya kufanikisha njama zao.

Njia nyingine mpya iliyobainika hivi karibuni ni pamoja na waporaji kuingia benki wakijifanya kuwa ni wateja lakini lengo lao likiwa ni kuwafuatilia watu wanaotoa fedha na pia, ipo njia nyingine inayowahusisha madereva wasio waaminifu na baadhi ya maofisa wa juu wa benki.

Aidha, Nipashe imebaini kuwa mbali na njia hizo mpya, zipo nyingine zilizoanza kutumika kitambo pia zinaendelea kutumika katika kufanikisha uporaji, zikiwamo zile za wenye bodaboda kunyakuwa mapochi na mikoba yenye fedha kutoka kwa wamiliki wake; kutumia taarifa kutoka kwenye mtandao maalumu unaohusisha baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wa benki na pia njia ya kinyama inayohusisha uvamizi wa ghafla na matumizi ya silaha za moto.

Kadhalika, zipo pia njia za kuwavamia watu na kuwashambulia kabla ya kuwapora fedha kwa namna sawa na ile inayoitumiwa na vikundi vinavyotambulika zaidi kwa jina la ‘panya road’.

Njia nyingine iliyozoeleka ni ile ya waporaji kuvamia maduka ya bidhaa au vibanda vya miamala ya fedha kupitia simu za mkononi na kushambulia kabla ya kupora kila senti wanayoikuta.

“Kwakweli hili suala la uporaji ni gumu na linataka ushirikiano wa kutosha kati ya polisi na wananchi… vinginevyo, matukio haya yataendelea kutokea kwa sababu waporaji wamekuwa wakitumia njia hizi mpya na nyingine nyingi wanazobuni karibu kila siku,” mmoja wa wafanyabiashara wa maeneo ya Manzese aliyewahi kukumbwa na tukio la kuporwa fedha aliiambia Nipashe kwa sharti la kutoandikwa jina lake.

UPORAJI MBINU MPYA UNAVYOFANYIKA
Akizungumza na Nipashe, mjumbe mmojawapo wa Jumuiya ya Wamiliki wa Benki (TBA), Ineke Bussemaker, alisema njia mojawapo inayotumiwa sasa kufanikisha uporaji kwa wateja wao ndani au wanapotoka na fedha nje ni watu kujifanya wateja na kuingia benki kwa nia ya kushuhudia wateja wanaochukua fedha.

Alisema baada ya wahalifu kujua ni mteja gani huchukua fedha, hutumia njia wanazojua wenyewe kuwasiliana kwa haraka na kumfuatilia kabla ya kufanikisha uporaji.

Bussemaker alisema matukio ya uporaji hayapo tu Dar es Salaam na mikoa mingine nchini, bali ni changamoto ya dunia nzima na hivyo kinachotakiwa ni kuongeza tahadhari za usalama ikiwa ni pamoja na wateja kutumia zaidi njia za kielektroniki katika kufanya miamala yao.

Mjumbe huyo wa TBA alisema kwa mtazamo wake, haamini kuwa kwa kiasi kikubwa jambo hilo hufanikishwa na watumishi wa benki.

Njia nyingine iliyobainika hivi karibuni ni ile ya kutumika kwa madereva wasio waaminfu wa maofisa wa benki.

Akizungumza na Nipashe, Kamanda wa Kanda Malumu ya Dar es Salaam, Simon Siro, alisema jambo hilo wamelibaini hivi karibuni baada ya tukio la uporaji lililohusisha benki moja kwenye Manispaa ya Kinondoni.

Alisema baada ya uchunguzi wao, wamefanikiwa kumkamata dereva wa Mkurugenzi wa Benki hiyo baada ya kupata taarifa zinazomhusisha na ujambazi huo.

“Huyo dereva mara nying alikuwa anakaa nje ya benki… akiona mtu amechukua fedha anawapigia simu waporaji.

Tumekwenda kwake kumkagua, tumekuta anamiliki vitu vya thamani kubwa yakiwamo magari, kuliko hata kipato chake,” alisema Kamanda Siro.

Kamanda Siro alitoa angalizo kwa wananchi kuongeza tahadhari za kiusalama pindi wanapochukua fedha huku pia akisema kuwa wamejipanga kuhakikisha kuwa uhalifu huo unadhibitiwa.

“Uhalifu huu ulikuwa umekoma lakini siku za karibuni umeanza kuibuka,” alisema na kuongeza:

“Pamoja na haya yote, jeshi litahakikisha mtandao wote unamalizwa ili kukomesha uhalifu huu.”

Njia nyingine iliyobainika hivi karibuni, ni ya kundi la waporaji wanaotumia bodaboda kuifukuzia gari wanayojua kuwa ina fedha na kumsimamisha dereva wakidai kuwa amemgonga mtu.

Akizungumza na Nipashe, ofisa mmoja wa kampuni binafsi ya ndege alisema yeye nusura aporwe kwa njia hiyo hivi karibuni wakati akipita maeneo ya Makongo Juu.

“Zilinijia bodaboda kwa kasi na kunifuata kwa mbele wakidai kuwa nimemgonga mwenzao.

Wakata niwafuate, lakini mimi nikakakataa na kuendesha gari huku nikiwaambia wanifuate polisi… cha kushangaza, hawakunifuata na badala yake wote kwa pamoja wakaondoka zao.

Ndipo baadaye nikabaini kuwa ni waporaji baada ya kufika polisi na kuambiwa kuwa nina bahati, hiyo ni moja ya mbinu mpya inayotumiwa sasa,” alisema ofisa huyo wa kampuni ya ndege.

Katika njia nyingine ya nne, inaelezwa kuwa waporaji hujibanza pembezoni mwa barabara zinazokuwa na foleni na kisha mmoja wao hulifuata gari wanaloamini kuwa limebeba fedha na kufanya hila ya kumgongea dereva kwa kujifanya wanataka kumwambia jambo.

“Baada ya hapo, kinachofuatia ni mporaji kujiingiza garini ghafla akiwa anatoa silaha na kumuamuru dereva afanye anavyotaka … wakati mwingine wenzake pia hujitokeza na kufanikisha njama zao,” alisema Shafii Iddi, dereva wa gari linalochukua wanafunzi katika Shule ya Msingi Sheikhati Hissa iliyopo Magomeni Mapipa aliyedai kuwa yupo rafiki yake aliyekumbwa na tukio la aina hiyo.

Akizungumzia namna ya kuepuka vitendo vya uporaji, hasa kwa njia hizo mpya na nyingine zilizozoeleka, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Johnson Minja, alisema ni wakati muafaka sasa kwa kila mfanyabiashara kufanya miamala yake kwa njia za kielektroniki na kwamba, kinyume chake ni kujihatarishia maisha.

Alipoulizwa ni sababu gani wafanyabiashara wengi hawapendi kutumia njia hiyo, Minja alisema wengi huogopa kufahamika na Serikali juu ya kiasi halisi cha fedha wanachomiliki, na hiyo kusabaisha baadhi ya wafanyabiashara kuhamisha fedha kutoka katika biashara zao kwenda nyumbani; jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao na fedha zao.

“Wengi huwa hawapendi kufahamika viwango vyao vya kuhamisha na kuweka fedha, ndiyo sababu wanapenda kutembea na kiasi kikubwa cha fedha, hali inayowasabisha wengi wao kuporwa… mambo yamebadilika sana. Ni vizuri wakafanya miamala yao kwa njia za kielektroniki,” alisema Minja.

Kadhalika, Minja alitoa wito kwa watoa huduma katika taasisi za fedha kwa wateja kuwa waadilifu na kufuata misingi na maadili ya taaluma zao kwa kuficha siri za wateja.

WAZIRI MAMBO YA NDANI
Akizungumza na Nipashe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema jeshi hilo limefanya mambo mengi kuhakikisha raia na mali zao wanakuwa salama.

Alisema hadi sasa kuna idadi kubwa ya askari mitaani wanaohakikisha kuwa usalama wa raia na mali zao unaimarishwa kote, na kwamba lililo muhimu ni kwa wananchi kutekeleza pia wajibu wao wa kushirikiana na jeshi la polisi kudhibiti uhalifu.

Kwa mfano, Mwigulu alisema siyo sawa hata kidogo kwa wananchi kukimbia na kujifungia ndani kwa kuogopa vikundi vya vijana maarufu kama ‘panya road’ bali kushirikiana katika kuwadhibiti kabla ya polisi kufika kwa sababu haiwezekani kukawa na askari katika kila mtaa.

“Haiwezekani mkasema panya road wamekuja kwenye mtaa wapo wanne, watano au 10 halafu wakanyamazisha mtaa mzima…wengine hawana hata silaha, wanakuja tu na vinanii hivi vya jadi (silaha za jadi) ambazo na sisi tunazo, halafu wananyamazisha mtaa mzima. Hii si lazima kusema tusubiri polisi, lazima tupambane kuhakikisha hatuachi wahalifu kutawala maeneo yetu,” alisema.

Alisema raia wakishirikiana na jeshi la polisi katika ulinzi, itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za matukio ya wizi na uporaji.

Matukio ya uporaji ya hivi karibuni ni pamoja na lile lililotokea Novemba 3 kwenye mataa ya kuongezea magari eneo la Super Star katika barabara ya Sam Nujoma ambapo watu waliokuwa na pikipiki walimpiga risasi kisha kumpora fedha Raia wa Uturuki, Erhan Copkur.

Mwezi wa uliopita katika kampuni ya kuuza vipuri vya mabasi ya Yutong iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, majambazi wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki mbili, walivamia na kupora fedha baada ya kumfuatilia mtu aliyetoka kuchukua fedha benki, kiasi cha dola 40,000 (Sh. milioni 80).

Oktoba mwaka huu, panya road walifunga mtaa wa Jitegemee uliopo Kimanga Tabata, Ilala jijini Dar es Salaam na kupora fedha kwenye vibanda vinavyotoa huduma ya fedha kwa kutumia simu na maduka yaliyo eneo hilo.

Septemba, 2016, majambazi wenye silaha walimuua kwa risasi askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na baadaye kumpora fedha Sh milioni tano, nje ya geti la nyumbani kwake Mtaa wa Kimanga, Tabata, saa tano asubuhi.

Habari Kubwa