Mbinu mpya za makahaba kukwepa mkono wa polisi

21Sep 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Mbinu mpya za makahaba kukwepa mkono wa polisi

NI mbinu mpya. Ndivyo inavyoweza kuelezwa kutokana na wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba kubuni mbinu mpya za kuwanasa wateja na wakati huo huo kukwepa mkono wa dola.

Hiyo inatokana na kamatakamata ya wanawake hao maarufu kama makahaba  katika Jiji la Dodoma, baada ya nyumba ya kulala wageni ya Keko iliyokuwa ikitumiwa kwa biashara hiyo kufungwa.

Katika kuhakikisha hawaondoki katika ulingo, wamebuni mbinu mpya tatu za kufanya biashara hiyo. Mbinu hizo ni pamoja na kuwasiliana na wateja wao kwa njia ya simu, kukaa kwenye baa na kumbi za starehe wakisubiri wateja na kukodi bodaboda kuzunguka nao kwenye maeneo waliyokuwa wakifanyia biashara kutafuta wateja.

Katika uchunguzi uliofanywa na Nipashe, maeneo yaliyokuwa yakitumiwa na makahaba yamefungwa ikiwamo gesti hiyo maarufu, huku wao wakibuni mbinu zingine za kuendelea kufanya biashara hiyo.

Pia kwa sasa wamekuwa wakiwinda wateja wao kwa kwenda kwenye baadhi ya baa kubwa na kununua kinywaji ambacho anakaa nacho kwa muda mrefu bila kuisha.

Sambamba na hilo wamekuwa wakirandaranda kwenye maeneo waliyokuwa wakiyatumia kwa usafiri wa pikipiki ili wasiweze kukamatwa na polisi.

Pamoja na kutumia mbinu hizo, gazeti hili limeshuhudia Jeshi la Polisi likiwa limeimarisha doria mitaa ya Uhindini na Airport nyakati za usiku ili kudhibiti biashara hiyo.

Walishindwa kulala

Mmoja wa wakazi wa Uhindini (jina limehifadhiwa), alisema kabla ya kamata kamata ya wanawake hao, hali ilikuwa mbaya kwa kuwa walikuwa wakishindwa kulala kutokana na kuwapo na kelele na kujiuza hadharani.

"Mimi nilikuwa nashindwa kulala usiku maana huu ndio mtaa waliokuwa wakiutumia. Tulilazimika kukesha nao usiku kucha na nikiingia kazini nashindwa hata kufanya kazi zangu kwa ufanisi," alisema.

"Kondomu na tishu zilikuwa zinazagaa hadi getini kwangu kwa hiyo nikiamka nalazimika kufanya usafi na kuokota." Aliongeza.

Alisema anamshukuru Mungu kwa jitihada zilizofanyika kwa kuwa takribani miaka minne alikuwa akipata adha ya kuwapo kwa biashara hiyo jirani na nyumba yake.

"Namshukuru Mungu sana kwa jitihada ambazo zimefanyika. Nilikuwa nashangaa muda mrefu kama kweli serikali ipo kwa nini isipige marufuku maana walikuwa wanasombwa na polisi baada ya saa mbili wanarudi. Lakini kilichofanyika kwa sasa ni miujiza kwa kweli tunalala vizuri," alisema.

Aliwashauri wanawake hao wafanye biashara ndogo ndogo badala ya kuuza miili kwa kuwa inamdhalilisha mwanamke.

MWENYEKITI WA MTAA

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tofiki, Alnoor Visram, alikiri kufungwa kwa nyumba ya kulala wageni katika mtaa huo kutokana na madada poa (makahaba).

"Mmoja wa wamiliki alikuja kwangu kunijulisha kuwa gesti yake anaifunga na barua anapeleka kwa Mkurugenzi wa Jiji na kuomba kugongewa muhuri na ilipofika siku ya pili kuangalia kweli nimekuta hata jina la gesti amelifuta nje," alisema.

Alisisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na polisi kuhakikisha biashara hiyo inadhibitiwa katika mtaa huo.

MEYA WA DODOMA

Alipoulizwa kuhusu jengo linalomilikiwa na jiji kulalamikiwa kuwa kijiwe cha makahaba, Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, alisema jengo hilo (CDA Club) linamilikiwa na jiji na kwamba limekodiwa na mtu ambaye wameingia naye mkataba wa kufanyia biashara.

Aidha, alisema wamebaini kuwa eneo hilo linatumika kwa biashara ya makahaba kama kijiwe cha makutano yao.

 "Zamani walikuwa wanatambulika kwa urahisi sana kwa sababu wanavaa nguo fupi, lakini kwa sasa wanavaa vizuri kistaarabu kabisa, lakini wateja wao wana mawasiliano nao," alisema.

Aliwataka wanaume kutowahitaji makahaba kwa kuwa uhitaji wao unasababisha kuwepo na biashara hiyo.

"Hawa makahaba ni watoa huduma kwa wahitaji sasa inatakiwa elimu itolewe na tuelimishe jamii kwamba hiki kitu kinahusu pande mbili, je, wateja wao tumefanya juhudi gani?" Alisema.

Prof. Mwamfupe alisema tatizo la makahaba linachangiwa na wanaume wanaowahitaji na kwamba katika jengo hilo biashara inayoendeshwa ni baa.

"Lile jengo tunaangalia mkataba na masharti ya biashara tuliyoingia nayo na kama kuna namna inakiukwa basi tutachukua hatua ikiwamo kuvunja mkataba," alisema.

WAHUKUMIWA KIFUNGO

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi liliwakamata na kuwafikisha mahakamani kwa nyakati tofauti makahaba 19 na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja kutokana na kupatikana na hatia ya  kufanya biashara hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema jeshi hilo linaendelea na msako wa kuwakamata makahaba katika maeneo mbalimbali wanaofanya kazi hiyo ya kujiuza kama sehemu ya kujiingizia kipato.

 

Alisema wanaofanya biashara hiyo wanatenda kosa hilo kinyume na kifungu cha Sheria namba 176 (a), (f) na (g) cha Kanuni ya Adhabu ya sura ya 16.

UDHIBITI UKAHABA

 

 Katika Mkutano wa 16 wa Bunge, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Maryam Msabaha, alisema katika majiji makubwa nchini likiwamo Dodoma, kumekuwapo na ongezeko la wanawake wanaofanya biashara ya kujiuza na kuhoji serikali ina mkakati gani hasa makao makuu ya nchi kudhibiti hali hiyo ili kupunguza ongezeko la kutupa watoto majalalani.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alisema Jeshi la Polisi limekuwa likifanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na watu wanaofanya biashara ya ngono na kuwataka wanaume kujiepusha kuwa wateja wa biashara hiyo.

Habari Kubwa