Mbivu, mbichi kesi vigogo CWT Mei 23

14May 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbivu, mbichi kesi vigogo CWT Mei 23

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajia kutoa uamuzi wa kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili aliyekuwa Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, na Mtunza Hazina Abubakar Allawi,  kama wana kesi ya kujibu au la Mei 23, mwaka huu.

Mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo jana baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao wa mashahidi tisa na vielelezo 11 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Richard Kabate.

Kesi hiyo kwa upande wa mashtaka, iliongozwa na Wakili Imani Nitume ambaye  aliwaongoza mashahidi hao mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa.

Seif na Allawi wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kujipatia zaidi ya Sh. milioni 13 kinyume cha sheria.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 3 hadi Novemba 6, 2018 jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kwamba washtakiwa wakiwa watumishi wa CWT, walitumia madaraka yao vibaya na kujipatia Sh. 13,930,963 kwa manufaa yao.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa katika tarehe na eneo hilo, washtakiwa  walichepusha kiasi hicho cha fedha mali ya CWT kwa kutumia nafasi walizo nazo.

Habari Kubwa