Mbivu, mbichi rufani ya Lema leo

20Dec 2016
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Mbivu, mbichi rufani ya Lema leo

JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Dk. Modesta Opiyo, leo anatarajiwa kutoa uamuzi wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), wa maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufani ya dhamana yake baada ya mahakama hiyo kutupa pingamizi mbili za upande wa Serikali.

Pingamizi za Serikali zilitupwa Desemba 16, mwaka huu na Jaji huyo baada ya kupitia hoja za pande zote na kusema kuwa pingamizi hizo za mawakili wa upande wa Serikali waliokuwa wakitaka maombi hayo yasikikilizwe, hazikuwa na hoja za kisheria zenye mashiko.

Katia maombi hayo namba 69, upande wa Serikali ulikuwa ukiwakilishwa na mawakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na Wakili Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.

Jana wakati akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi hiyo ili rufaa hiyo iweze kusikilizwa, Wakili Mfinanga alisema yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya kifungu 361(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alisema uamuzi unaotarajiwa kukatiwa rufaa ni uliotolewa Novemba 11, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Alitaja sababu mbili za msingi za kukatia rufaa uamuzi huo kuwa ni kuiomba Mahakama hiyo ipitie makosa ya kisheria yaliyofanywa na Mahakama ya chini na kusema kuwa uamuzi huo ulimpa mleta maombi (Lema) dhamana ila kabla hajapewa masharti ya dhamana, upande wa Jamhuri ulitoa notisi ya nia ya kukata rufaa.

Aliiomba mahakama hiyo iwape muda ambao hautazidi saa 1:30 kwa ajili ya kuleta notisi hiyo ili Mahakama iweze kurekebisha makosa hayo yaliyofanywa na Mahakama ya chini.

Akiwasilisha hoja ya pili, Wakili Mangula alidai mahakamani hapo kuwa tangu kutolewa kwa uamuzi huo hawajapumzika, muda mwingi walikuwa mahakamani kuomba kurekebishwa kwa makosa hayo ya kisheria.

Alisema Novemba 14, mwaka huu walipeleka barua ya malalamiko mahakamani hapo na walipoitwa, pande zote mbili katika shauri namba 6, walikumbana na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawakili wa Serikali.

Akijibu hoja za waleta maombi hao, Wakili Ngole alidai kuwa ni wazembe na kwamba hata uamuzi wanaolamlamikia mahakamani hapo ambao awali ulimpa mleta maombi dhamana lakini kabla hajapewa masharti ya dhamana, Mahakama iliingiliwa mamlaka yake hawajawasilisha na maombi hayo.

Wakili huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na makosa yoyote ya kisheria kama inavyodaiwa na waleta maombi hao na kudai kuwa baada ya hakimu kusema Mahakama inampa mshitakiwa dhamana, Jamhuri kwa haki yake, walisimama na kuifahamisha Mahakama kwamba wana nia ya kukata rufaa.

Lema yuko mahabusu kwa zaidi ya mwezi mmoja katika gereza Kuu la Kisongo baada ya kukamatwa Novemba 2, mwaka huu kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma kisha kufikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Magufuli.

Habari Kubwa