Mbivu, mbichi U-spika CCM

19Jan 2022
Maulid Mmbaga
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mbivu, mbichi U-spika CCM

MBIVU na mbichi ya wateule watatu watakaopitishwa kwa kupigiwa kura na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya Spika wa Bunge, itajulikana leo.

Mchakato huo unaendelea pia kwenye Chama cha ADC ambacho ni kati ya vyama vya upinzani chenye mgombea, Maimuna Kassim, aliyejitokeza kuchukua fomu ya kuwania kiti hicho kilichoachwa wazi.

Wateule ndani ya CCM watajulikana baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kupitisha majina matatu yatakayopelekwa kwa hatua zaidi.

Kamati hiyo iliyokutana jana na leo ndiyo inayokamilisha mchakato huo baada ya kupokea majina yaliyopitiwa na sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Sekretarieti hiyo ilikutana Januari 17, mwaka huu, kujadili na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa wagombea waliojitokeza kuomba kiti hicho.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa awali Januari 9, mwaka huu na Katibu Idara ya Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka, urejeshaji fomu ulikamilika Januari 15, mwaka huu.

Kabla ya kupigiwa kura na wabunge wote, Janauri 21 hadi 30 (wiki ijayo) kikao cha chama cha wabunge wa CCM (caucus), kitapiga kura kumpata mgombea ambaye atakwenda kuomba kura bungeni.

Hadi sasa wanachama wa CCM 71 wameomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo ya u-Spika.

Miongoni mwa waliojitokeza kwenye kijany’anyiro hicho ni Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Sophia Simba na aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa Jimbo la Bariadi (CCM) kwa muda mrefu, Andrew Chenge.

Makada wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni wabunge mbalimbali akiwamo Joseph Kasheku maarufu Msukuma, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Bunge la Afrika (PAP) na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele na mwingine ni msomi aliyejinasibu ana shahada tisa, Baraka Byabato.

Baada ya kukamilika kwa mchakato ndani ya chama hicho, jina litakalopitishwa litawasilishwa bungeni Februari mosi, mwaka huu, kwa ajili ya wabunge kuchagua Spika atakayepigiwa kura kushika nafasi hiyo.

Vile vile, mgombea huyo atakayepitishwa na CCM atashindana na wagombea wa vyama vingine kwa wingi wa kura za wabunge baada ya kujinadi mbele yao wakati wa vikao vya bunge.

Mchakato wa kumpata Spika mpya umeanza baada ya Spika Job Ndugai kujiuzulu nafasi hiyo Januari 6, mwaka huu, baada ya kauli yake ya kupinga mikopo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua taharuki hali iliyosababisha baadhi ya watu kushinikiza ajiuzulu nafasi hiyo kwa kile kilichoonekana kupingana na kiongozi wake.

Habari Kubwa