Mbobezi kodi ajitosa uspika wa Bunge

14Jan 2022
Faustine Feliciane
DAR ES SLAAM
Nipashe
Mbobezi kodi ajitosa uspika wa Bunge

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mtaalam mbobezi wa masuala ya kodi, Hamidu Chamani leo amerudisha fomu ya kugombea uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwenye ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam.

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mtaalam mbobezi wa masuala ya kodi, Hamidu Chamani.

Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kurudisha fomu hizo, Chamani amesema anaamini anao uwezo wa kuongoza Bunge na kukisaidia chama chake katika kuleta maendeleo ya nchi.

Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuwania nafasi ya uspika umekuja kufuatia Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu kwenye nafasi hiyo Januari 6 mwaka huu baada ya kuwepo kwa taharuki juu ya utata wa kauli zake juu ya mikopo inayochukuliwa na serikali chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kujiuzulu kwa Ndugai kumetoa nafasi kwa CCM kuruhusu wanaotaka kuwania uspika kupitia chama hicho kuchukua na kurudisha fomu kuanzia Januari 10 hadi 15, 2022 ambapo mpaka sasa makada 49 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Chamani aliwahi kuwania Ubunge wa jimbo la Kyerwa mkoani Kagera mwaka 2020 amesema idadi kubwa ya waliowania nafasi hiyo haimpi tabu kwa kuwa yeye ni bora zaidi yao.

"Nimefanya kazi za kukitangaza chama tangu mwaka 2010 nimehamasisha vijana wengi wa vyuo vikuu kujiunga na CCM wapo wengine niliowapatia kadi kwa mkono wangu, nikiwa chuoni nimetoa Kwa mkono na gharama zangu Kadi zaidi ya 500 Kwa vijana," alisema Chamani na kuongeza,

"Ninajiamini nakijua chama na nitatumika vyema kwenye nafasi ya uspika,” alisema Chamani ambaye kwa sasa ni msimamizi wa mashine za kutolea risiti kwa njia ya kielektroniki jijini Dar es Salaam.

Gharama ya fomu moja ni Sh. Milioni moja, hivyo idadi ya makada wanaowania nafasi hiyo inatarajiwa kuongezeka.Miongoni mwa makada wa CCM walipochukua aliochukua fomu ya kuwania uspika ni Katibu mstaafu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, Waziri wa zamani, Athuman Mfutakamba, Mussa Zungu, naibu Spika Tulia Ackson, mwanasheria mkuu wa zamani Andrew Chenge na mbunge wa Geita Joseph Kasheku 'Msukuma'.

Habari Kubwa