Mbowe abeba siri ya Lowassa Ikulu    

12Jan 2018
Mary Geofrey
Nipashe
Mbowe abeba siri ya Lowassa Ikulu    

WAKATI mijadala mbalimbali ikiendelea kuibuka kuhusiana na hatua ya aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kwenda Ikulu na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli, imebainika kuwa siri ya baadhi ya mambo yaliyozungumzwa na viongozi hao,-

Iko kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Lowassa alikwenda Ikulu, Dar es Salaam Jumanne na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli yaliyohusiana na masuala mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa jana kwa umma na msemaji rasmi wa Lowassa, Aboubakary Liongo, ndiyo iliyofafanua jambo hilo kwa kueleza kuwa Lowassa alimfikishia Mbowe mrejesho wa kile kilichozungumzwa baina yake na Rais Magufuli alipomtembelea Ikulu.

“Baada ya ziara ile, Mheshimiwa Lowassa alikutana na Mwenyekiti wa chama chake, Mheshimiwa Freeman Mbowe na kumpa mrejesho wa yaliyojiri Ikulu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya Liongo.

Taarifa hiyo ilikuwa na lengo la kukanusha taarifa mbalimbali zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia siku ya kufanyika kwa ziara hiyo ya Lowassa, Ikulu.

Vilevile, taarifa hiyo ilieleza kuwa taarifa rasmi juu ya mrejesho wa mazungumzo baina ya Lowassa na Rais Magufuli itatolewa kwa njia rasmi na watu wenye mamlaka hayo.

“Taarifa rasmi zitatolewa kwa njia rasmi na watu wenye mamlaka hiyo. Poleni kwa usumbufu wote. Mwisho tutayashinda haya kama tulivyoshinda mengine kwa umoja wetu,” iliongeza taarifa hiyo ya Liongo.

Jana, jitihada za kumpata Mbowe ili aelezee kwa undani taarifa kwamba anao mrejesho wa mazungumzo baina ya wawili hao, ziligonga mwamba baada ya simu yake kutopokewa licha ya kuita mara kadhaa.

Baadaye, katika kile kilichoonyesha kuwa huenda alikuwa katika mkutano au eneo lolote asiloweza kuzungumza, Nipashe ilipokea ujumbe mfupi wa maandishi kutoka simu ya Mbowe kumtaka mwandishi awasiliane naye kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu: "Please text me…”

Hata hivyo, baada ya mwandishi kumtumia ujumbe uliotaka ufafanuzi kuhusu madai kwamba anao mrejesho wa mazungumzo ya Lowassa akiwa Ikulu, hakukuwa na majibu.

Mbali na Chadema, vyama vingine vilivyowakilishwa na Lowassa kwa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ni vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).

Katika matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, Lowassa alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 39.97 ya kura halali zilizopigwa na kuweka historia kwa kuipa kura nyingi zaidi kambi ya upinzani tangu kuanza kufanyika uchaguzi unaohusisha vyama vingi mwaka 1995, huku Rais Magufuli akiibuka kidedea kwa kupata asilimia 58.46 ya kura hizo.     ILIVYOKUWABaada ya Lowassa kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli, picha zilimwonyesha akiwa mwenye furaha tele na mwenyeji wake kuashiria kile kilichoelezewa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa ni uthibitisho kuwa ‘siasa si uadui’.

Kisha, taarifa iliyotumwa baadaye na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilieleza namna Lowassa alivyomwelezea Magufuli na pia Rais alivyomsifu Lowassa. Pia video zilizosambazwa na Ikulu zilionyesha namna kila mmoja anavyomkubali mwenzake katika namna mbalimbali.  

Lowassa alimpongeza Rais Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano kwa kufanikisha masuala kadhaa ya maendeleo na kushauri kuwa awe akitiwa moyo, akiyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni utoaji elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne; kutengeneza ajira kwa kuanza miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) na mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge; usambazaji zaidi wa umeme vijijini na pia usambazaji wa huduma za maji.

Katika kikao hicho, Rais Magufuli alimwelezea Lowassa kuwa ni mwanasiasa aliyefanya mengi ya manufaa kwa taifa na akampongeza kwa kuendesha kampeni za kistaarabu zisizokuwa na chembe ya matusi dhidi yake wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Baada ya tukio hilo la Lowassa kukutana na Rais Ikulu, baadhi ya viongozi wa Chadema walitoa maoni tofauti ya kupinga kile alichokieleza, akiwamo Mbowe aliyesema kwenda Ikulu si tatizo bali kilichozungumzwa na mwanachama mwenzao huyo si msimamo wa Chadema.

Baadhi ya wabunge wa chama hicho, wakiwamo Tundu Lissu wa Singida Mashariki, Godbless Lema (Arusha) na Saeed Kubenea (Ubungo), pia walikaririwa wakitoa maoni tofauti yaliyoashiria kutompinga Lowassa kwenda Ikulu, lakini kutokubaliana na kile alichokieleza.

Jana, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Julius Mwita, alisema hawana uhakika kama Lowassa aliwasiliana na Mbowe na kwamba hawapingi hatua yake ya kukutana na Rais Mgufuli bali kile alichosema baada ya mazungumzo yao hayo.

Mwita alisema tatizo ni kauli aliyoitoa Lowassa ya kuisifu serikali ilhali ndani ya nchi kuna changamoto mbalimbali zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi.

UFAFANUZI KAMILI WA LOWASSA

Ifuatayo ni taarifa kamili iliyotolewa na msemaji wa Lowassa, Liongo, kuelezea ziara yake kwenda Ikulu na pia kukanusha baadhi ya taarifa zinazosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii;

Kumekuwa na waraka na taarifa nyingi za kupotosha umma kuhusu ziara ya Mheshimiwa Edward Lowassa kwenda Ikulu na nyingine zikisemwa zimetoka kwa msemaji wake. Taarifa zote hizo siyo kweli na wala siyo rasmi kutoka ofisini kwa Mheshimiwa Lowassa.

Baada ya ziara ile, Mheshimiwa Lowassa alikutana na Mwenyekiti wa Chama chake, Mhe. Freeman Mbowe na kumpa mrejesho wa yaliyojiri Ikulu.

Kumekuwa na taarifa nyingi kwenye mitandao zikiwamo kufunguliwa kwa akaunti mbalimbali feki, taarifa zote hizo zipuuzwe kwani zina lengo la kupotosha kwa malengo wanayoyajua wapotoshaji hao pamoja na mawakala wao.

Taarifa rasmi zitatolewa kwa njia rasmi na watu wenye mamlaka hiyo. Poleni kwa usumbufu wote. Mwisho tutayashinda haya kama tulivyoshinda mengine kwa umoja wetu.

Aboubakary Liongo,Msemaji Rasmi wa Mhe. Edward Lowassa.