Mbowe akana kutuma mawakala kuandamana

09Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mbowe akana kutuma mawakala kuandamana

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, katika siku yake ya tatu ya utetezi, amekana mahakamani kutoa maelekezo kwa mawakala wa chama chake kufanya maandamano kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kufuata nakala za barua za utambulisho.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akisalimiwa na viongozi wengine baada ya kupata mapumzimko wakiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: MIRAJI MSALA

Mbowe alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakumu Mkazi Mkuu Thomas Simba, wakati akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande, kuhusu kuwaagiza mawakala wake kufanya maandamano kwenda kwa Mkurugenzi.

Alidai kuwa siku ya tukio wakati wanamaliza mkutano wa kampeni, mawakala wa chama chake walikuwa hawajapata barua za utambulisho, hivyo aliwataka wafuatilie kwa amani.

"Niliwataka mawakala wafuatilie barua hizo sijui kama walitii au hawakutii kwa sababu walikuwa na taharuki kwa kukosa vitambulisho hivyo," alidai Mbowe.

Wakati akihojiwa na wakili wa serikali Jacqueline Nyantori, Mbowe alidai hakuwapo wakati wa matukio ya kifo cha Mwangozi, msaidizi wake Ben Sanane na aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu bali alisikia kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii ikiwemo JamiiFolam.

Alidai Jamiifolam si chombo cha uchunguzi na hakuwahi kuthibitisha taarifa hizo kama vyombo vya ulinzi na usalama vilihusika katika matukio hayo.

Mbowe pia alidai katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni, chama chake kilishiriki na kilitia saini mwongozo wa maadili ya uchaguzi wa mwaka 2015 na ni sahihi mwongozo huo unaeleza namna ya vyama vya siasa kukosoana.

Alidai Februari 16, 2018 Chadema ilihitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni katika Kiwanja Cha Buibui Mwananyamala na polisi ni miongoni mwa watu waliokuwapo katika mkutano huo.

Wakati akihojiwa na Wakili wa Serikali Salim Msemo, Mbowe aliieleza mahakama kuwa Jeshi la polisi ndilo linahusika na masuala ya kiupelelezi na hafahamu kama kuna idara ya upelelezi katika jeshi hilo.

Alidai kuwa wakati akitoa ushahidi wake mahakamani moja ya kesi alizotaja ni kuhusu kifo cha Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi na anaamini upelelezi wa shauri hilo ulifanywa na jeshi la polisi.

Mbowe alidai hana taarifa kama suala la kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wao wa hamasa Geita, Alphonce Mawazo, limeshafikishwa mahakamani na hoja za awali zilisomwa Agosti 28. mwaka huu.

Kesi hiyo imepangwa kuendelea mfululizo kuanzia Novemba 13 hadi 15, mwaka huu ambapo Mbowe ataendelea kuhojiwa na mawakili wa serikali.

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; na Mbunge wa Kawe Halima Mdee.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwamo la kula njama na kwamba wote wanadaiwa kuwa kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam waliku─║a njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Habari Kubwa