Mbowe amuomba Samia tume ya ukweli, upatanishi

10Jun 2021
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Mbowe amuomba Samia tume ya ukweli, upatanishi

​​​​​​​MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan, kuunda tume ya upatanishi, ukweli na maridhiano ili isikilize vilio vya Watanzania walioumizwa na kuteswa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

​​​​​​​MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe,

Amesema hatua ya kuunda tume hiyo ni kutoa fursa na nafasi kwa watu kutoka makundi mbalimbali kujitokeza kusema ukweli Ili waliofanya makosa waombe radhi ili matukio hayo yasijirudie.

Mbowe alitoa ombi hilo wakati wa mkutano wa Baraza la Mashauriano wa CHADEMA Mkoa wa Morogoro uliowashirikisha viongozi wa chama hicho kutoka majimbo 11 ya uchaguzi ya mkoa huo.

Alisema baada ya kuundwa tume hiyo na watu kupewa nafasi ya kuwasilisha madhila walioyapata, itasaidia waliofanya makosa waliombe radhi Taifa ili kufikia maridhiano ya pamoja.

Kwa mujibu wa Mbowe, yapo makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi, viongozi wa dini ambao wameumizwa na baadhi ya viongozi waliokuwa madarakani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alisema kukamatwa kwa aliyekuwa kiongozi mmoja wa serikali hivi karibuni na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali, sio suluhisho la vilio vya Watanzania wengi walioteswa na baadhi ya viongozi waliokuwa serikalini kipindi hicho.

“Wapo viongozi na watumishi kutoka taasisi mbalimbali, na sehemu nyingine wamewaumiza sana Watanzania katika kipindi hicho cha miaka mitano iliyopita wajitokeze kuliomba radhi taifa hili ili tuishi kwa maridhiano,” alisema Mbowe.

Alisema hakuna sababu ya kukwepa kuundwa tume hiyo kwa kuwa waliofanya hivyo mpaka sasa wapo katika serikali na wanaendelea kufanya kazi bila shaka yoyote.

Aliongeza kuwa amani ya nchi hii na utengamano vitapatikana pale tu ukweli utakapobainika kutoka kwa viongozi ili kupukana kujenga taifa lenye visasi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAWACHA), John Pambalu, alimuomba Rais Samia atakapokwenda Mwanza kuwaambia vijana atawaachia lini wafungwa wa kisiasa, ambao alidai wengi wao wamebambikiwa kesi.

Habari Kubwa