Mbowe apangua Baraza la Mawaziri Kivuli

03Apr 2020
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe
Mbowe apangua Baraza la Mawaziri Kivuli

KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amefanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri ikiwa imebaki takribani miezi mitatu kufika ukomo wa Bunge la 11.

KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, picha mtandao

Bunge hilo linatarajiwa kuvunjwa na Rais John Magufuli Juni 30, mwaka huu.

Taarifa ambazo Nipashe ilizipata jana kutoka ndani ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kuthibitishwa na baadhi ya mawaziri kivuli, zilieleza kuwa mabadiliko hayo yalifanywa juzi jijini Dodoma.

Baraza hilo lina mawaziri 21 na wote safari hii wametoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mawaziri kivuli ni pamoja na Jaffari Michael (Moshi Mjini) anayekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, akisaidiwa na Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, anakuwa Ruth Mollel ambaye ni waziri pekee asiyekuwa na msaidizi (naibu waziri).

Tunza Malapo (Viti Maalum) atakuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akisaidiwa na Zainabu Mussa Bakar wakati Esther Bulaya akiendelea kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Ajira na Vijana), akisaidiwa na Frank Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma.

Wizara ya Kilimo itakuwa chini ya Pascal Haonga, Mbunge wa Mbozi, akisaidiwa na Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest, wakati Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiendelea kuwa chini ya Dk. Immaculate Sware anayesaidiwa na Lucy Mageleli.

Katika baraza hilo, Qambalo Qulwi ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akisaidiwa na Suzan Kiwanga, Mbunge Mlimba mkoani Morogoro.

Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea kuwa chini ya Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, akisaidiwa na Catherine Ruge wakati Wizara ya Nishati sasa inaongozwa na Grace Tendega na Naibu Waziri Jesca Kishoa.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, sasa anakuwa Waziri wa Madini akisaidiwa na Joseph Haule 'Prof Jay' wakati Wizara ya Katiba na Sheria ikiwa chini ya Salome Makamba na Naibu Waziri, Sabrina Sungura.

Wizara ya Maliasili na Utalii inaongozwa na Mch. Peter Msigwa akisaidiwa na Joyce Mukya huku Wizara ya Ulinzi ikikabidhiwa kwa Gibson Meiseyeki na Naibu Waziri Peter Lijualikali.

Wizara ya Mambo ya Ndani na ile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, zitakuwa chini ya mawaziri Godbless Lema (hajabadilishwa) na Esther Matiko (hajabadilishwa) wakisaidiwa na Rhoda Kunchela na Upendo Peneza, mtawalia.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inaongozwa na Wilfred Lwakatare na Naibu Waziri Grace Kiwelu wakati Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itakuwa chini ya David Silinde aliyehamishwa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango alikokuwa Naibu Waziri. Silinde atasaidiwa na Lucy Owenya.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inaendelea kuwa chini ya Waziri Susan Lyimo akisaidiwa na Yosepher Komba, aliyechukua nafasi ya Birago Kasuku aliyefariki dunia.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri ni Cecilia Paresso na Naibu Waziri Hawa Mwaifunga wakati Wizara ya Maji ikiwa chini ya Zubeda Sakuru akisaidiwa na Lucy Mlowe huku Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Muchezo ikiendelea kuwa chini ya Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Naibu Waziri yule yule Devotha Minja.

Wakizungumzia mabadiliko hayo jana, Mchungaji Msigwa na Lyimo walisema yamefanyika kwa kuzingatia vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kujaza nafasi zilizokuwa wazi kutokana na kujiuzulu kwa baadhi ya wabunge wa upinzani.

Lyimo pia alisema mabadiliko yamefanywa ili kuwaondoa mawaziri ambao tayari wameshaweka wazi kuwa na mpango wa kuachana na Chadema, akimtolea mfano Antony Komu ambaye alikuwa Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Habari Kubwa