Mbowe asononeka kuondoka Lowassa

16Mar 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mbowe asononeka kuondoka Lowassa

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu kuondoka kwa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama hicho, Edward Lowassa, kurudi CCM.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu miezi mitatu aliyokaa gerezani na kudidimia kwa demokrasia nchini. Kushoto kwake ni Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko. PICHA: MIRAJI MSALA

Akizungumzia hatua hiyo ya Lowassa, Mbowe amesema imemsikitisha sana.

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, mwaka 2015 alipeperusha bendera ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF), NCCR Mageuzi, DP, NLD na Chadema yenyewe.

Wakati Lowassa akitangaza kurudi CCM Machi Mosi, mwaka huu, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, walikuwa mahabusu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mambo mbalimbali, Mbowe alisema kitendo cha Lowassa kuondoka Chadema na kurudi CCM, kimemsikitisha kwa sababu walimpokea kwa nia njema.

“Habari za kuondoka nilizipata nikiwa gerezani kwa kweli nilisikitika. Nilisikitika kwa sababu tulimpokea kwa nia njema,” alisema Mbowe.

Kutokana na kitendo hicho, Mbowe alimtaka Lowassa akaseme ukweli huko aliko ili akisaidie chama tawala.

“Lowassa akaseme ukweli na akisaidie chama chake kipya kisiendelee kuwatesa Watanzania, sisi tutaendelea kuijenga demokrasia na Chadema hatutajenga chama chenye visasi wala hakitamwaga damu za watu,” alisema.

Mbowe alisema wakati wa uhai wake, Mwasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema chama cha siasa ni dodoki ambalo ukiliweka kwenye maji litanyonya maji, likiwekwa kwenye maziwa litanyonya maziwa na hata likiliwekwa kwenye maji taka litayanyonya.

Alisema Chadema kikiwa chama cha siasa, wajibu wake mkubwa ni kukijenga na kuongeza wanachama ndiyo maana mwaka 2015 walimwongeza Lowassa kwenye safu yao.

“Nataka nilizungumze kwa kifupi sana. Vyama vyetu vya siasa vinavuta watu wa makundi mbalimbali. Wapo watu wema na wasio wema, wapo watu wenye kupenda madaraka, wapo wanaotumwa na kuendeshwa na wivu wa  kuwatumikia watu na kutumikia taasisi,” alisema.

Aliongeza: “Kila mmoja katika uelewa wake anajua anataka nini katika chama cha siasa. Ingawa meza hii tuko Chadema watupu inawezekana miongoni mwetu tuna ajenda za ziada.”

Hata hivyo, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema katika siasa inahitaji kujitolea kwa sababu kazi hiyo ni ngumu.

“Wako tulioanza nao wakashindwa katikati, wako tuliowakuta katikati tumeenda nao lakini wakashindwa, kila mmoja na sababu zake. Kwa sababu lengo letu ni kusimamia haki, yeyote ambaye wajibu huo ameona ni mzito ni bora asiwepo,” alisema.

“Unapoona maovu yanafanyika usikemee, unapoona watu wanafungwa bila sababu usitoe tamko, unapoona watu wanapotea na wewe ukaona ni haki na kukaa kimya unapoona watu wanapigwa risasi, huoni kwamba ni uovu, ni bora ukishindwa kulia na sisi, usiwe na sisi,” aliongeza.

Kuhusu mambo yanayoendelea CUF, Mbowe alisema anawaombea wamalize kile wanachokifanya.

“Nimemsoma Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, anatutuhumu Chadema. Siwezi kubishana naye hata kama sikubaliani na siasa zake, namtakia heri huko alikoamua kutumikia, kama anatumikia wananchi tutajua muda ukifika,” alisema.

Pia alimweleza Maalim Seif Sharif kuwa haki ya Zanzibar iliyopokwa itarejea siku moja na kwamba anamwombea mema yeye na timu yake na wanalia pamoja kwa yanayoendelea.

Akizungumzia kuhusu Bunge kutangaza kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, amepoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge, Mbowe alisema si kweli kwamba mbunge huyo hakuhudhuria vikao hivyo mfululizo.

“Kambi ya upinzani bungeni ni ofisi, hata nikiwa magereza bado ofisi ipo, nilitarajia kwa tukio kubwa kama hili tufahamishane.

“Mimi kama kiongozi nimesoma habari hizi kwenye mtandao, sina taarifa na Jumanne nilikuwa Dodoma nikakutana na Spika Job Ndugai kama Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni nikahoji mambo mbalimbali na changamoto lakini hili sikuelezwa. Nimemwambia Nassari azungumze leo (jana) kuhusu suala hili,” alisema.

ASIMULIA HALI GEREZANI

Katika hatua nyingine, Mbowe alisema hali ya magereza nchini si ya kuridhisha kutokana na mrundikano wa mahabusu na wafungwa baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya miezi mitatu.

Alisema katika magereza kuna ugonjwa wa ngozi ambao husababishwa na kunguni na chawa ambao chanzo chake ni uchafu uliokithiri.

"Ugonjwa huu wanauita burudani kwa sababu mtu ukilala unajikuna sana mwisho wa siku unaathiri viungo vya mwili. Kule magereza mtu anaweza kukaa wiki hajaoga na wanalala godoro futi tatu watu wanne,” alisema.

Mbowe alisema mrundikano huo wa mahabusu magerezani unatokana na upelelezi na uchunguzi wa kesi zao kutokamilika kwa wakati.

"Mfano kesi za ugaidi wakifikishwa mahakamani wanaambiwa upelelezi unaendelea, watu hawa wanalalamika, wanafutiwa mashtaka na kufunguliwa mashtaka mapya,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba Jaji Mkuu, Jeshi la Polisi na Kamishna wa Magereza wafanye operesheni ya kusafisha miundombinu hiyo.

“Mkakati mahsusi wa kuondoa nusu ya mahabusu wanaooza kwenye magereza ufanyike, kitu kinachoitwa upelelezi unaoendelea umetumika kama mwamvuli wa kuficha uwazi wa kufanya uchunguzi,” alisema.

Aidha, Mbowe aliviomba vyombo husika kutafakari kuhusu suala hilo kwa sababu wakifanya hivyo watatambua nusu yao hawana kesi.

Mbowe aliomba mahakama za mwanzo zimulikwe sana kwa sababu watu hawapati haki zao kwa wakati.

Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, alisema ameona ombaomba wengi huko na kwamba watu wenye matatizo ya akili wanachanganywa na wa kawaida ambapo jambo hilo ni hatari.

Habari Kubwa