Mbowe, wenzake wasomewa upya mashtaka

15Mar 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mbowe, wenzake wasomewa upya mashtaka

VIGOGO  tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanaokabiliwa na kesi ya  uchochezi na kufanya mkusanyiko usio halali akiwamo Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Freedman Mbowe, wamesomewa upya mashtaka.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) taifa, Freeman Mbowe (wa tatu kulia) akiwa na viongozi waandamizi wa chama wakati kesi yao ilipotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: MIRAJI MSALA

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
 
Hakimu Simba alisema amepangiwa kusikiliza kesi hiyo baada ya hakimu wa awali kuhama kituo cha kazi na sasa jalada limehamishiwa mbele yake.
 
"Kwa kuwa kesi hii imehamishiwa kwangu washtakiwa watakumbushwa kwa kusomewa mashtaka yao upya kabla ya kuendelea kusikiliza ushahidi wa Jamhuri na tutaanza Machi 28 na 29, mwaka huu "alisema Hakimu Simba.
 
Mapema mahakamani hapo upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Simon Wankyo akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Patrick Mwita, ulidai kuwa washtakiwa wote wapo na kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa.
 
Wankyo aliwakumbusha washtakiwa mashtaka yao na wote kwa nyakati tofauti waliyakana.
 
Upande wa Jamhuri uliomba mahakama kurejea amri ya Mahakama Kuu iliyokuwa imeketi chini ya Jaji Rumanyika Machi 7, mwaka huu, kwamba kesi hii iendelee kusikilizwa.
 
"Mheshimiwa tunaomba tarehe ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri ili tuanze kuita mashahidi,"alidai Wankyo.
 
Upande wa utetezi ukiongozwa na jopo la mawakili Profesa Abdalah Safari, Jeremiah Mtobesya, Hekima Mwasipu, Peter Kibatala na John Mallya, uliomba mahakama ipange tarehe za kusikiliza bila kuingiliana na ratiba zao za Mahakama Kuu.
 
"Tumeshalipwa na wateja mheshimiwa hakimu hatuwezi kuacha kwenda kusikiliza kesi Mahakama Kuu kwa ajili ya kesi hii moja," alidai Profesa Safari.
 
Hata hivyo, Hakimu Simba alisema mahakama yake haiwezi kufanya kazi kwa kufuata ratiba ya utetezi.

"Mnatakiwa mjipange kesi hii ina mawakili wengi usipokuwapo wewe wengine watakuwapo kuendelea na kesi, tunafanya kazi ya utoaji haki kwa mujibu wa sheria," alisema Hakimu Simba.
 
Alisema mahakama yake itasikiliza ushahidi wa Jamhuri Machi 28 na 29, mwaka huu dhamana ya washtakiwa inaendelea.
 
Mbali ya Mbowe washtakiwa wengine ni Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko;  Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe,  Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini,  John Heche na Mbunge wa Bunda,  Ester Bulaya.
 
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka jana, wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.
 
Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka jana, Bulaya alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni,jijini  Dar es Salaam alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.
 
Pia ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka jana katika barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni wilaya ya Kinondoni, washitakiwa kwa pamoja na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa jeshi la polisi Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.
 
Siku ya tukio la kwanza na la pili, ilidaiwa kuwa katika viwanja vya Buibui vilivyoko Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara, Heche alitoa lugha ya  kuchochea chuki akitamka kwamba: "Kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii...wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano...watu wanapotea...watu wanauawa  wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome."

Maneno hayo yanadaiwa kuwa yalielekea kuleta chuki kati ya serikali na Watanzania. Washtakiwa wote waliposomewa mashtaka yao kwa nyakati tofauti walikana.