Mbunge ahoji kodi huduma milioni 800 kuyeyuka

28Feb 2020
Marco Maduhu
Shinyanga.
Nipashe
Mbunge ahoji kodi huduma milioni 800 kuyeyuka

Mbunge wa Vitimaalumu mkoani Shinyanga kupitia Chadema, Salome Makamba, amehoji juu ya kuyeyuka kwa ulipwaji wa kodi ya huduma Shilingi Milioni 800, fedha ambazo zilipaswa kulipwa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kutoka kwenye viwanda vya wachina.

Mbunge wa vitimaalum mkoani Shinyanga kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema Salome Makamba akizungumza na waandishi wa habari.

Makamba alibainisha hayo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari, juu ya kutolipwa kwa fedha hizo na kuendelea kusua sua kwa ukamilishwaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga, ukiwamo mradi wa machinjio ya kisasa, dampo, pamoja na Mazingira Center eneo la uwekezaji kibiashara.

Alisema kume kuwapo na sinto fahamu juu ya ulipwaji wa kodi hiyo ya huduma kutoka kwenye viwanda vya wachina Shilingi Milioni 800, ambapo alijaribu kufuatilia kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ili kujua hatima ya ulipwaji wa fedha hizo, lakini hakupewa majibu, pamoja na ukamilishwaji wa miradi hiyo ya maendeleo.

“Niliandika barua kwa Mkurugenzi wa Mansipaa ya Shinyanga, ili nipate ufafanuzi juu ya hatimaye ya ulipwaji wa kodi ya huduma Shilingi Milioni 800 kutoka kwenye viwanda vya wachina, pamoja na kusuasua kwa ukamilishwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ili nione namna ya kusaidia lakini sikupata majibu,”alisema Makamba nakuongeza;

“Hivyo nimeona njia nyingine rahisi ya kupata majibu yangu ni kutumia vyombo vya habari, ndio maana nimewaita hapa ili mnisaidie kupata majibu ya maswali yangu kutoka kwa Mkurugenzi, juu ya hatima ya ulipwaji wa kodi ya huduma Shilingi Milioni 800 kutoka kwenye viwanda vya wachina,”alisema 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Geofley Mwangulumbi, alitolea ufafanuzi juu ya suala hilo la ulipwaji wa kodi ya huduma kutoka kwenye viwanda cha wachina, kuwa wawekezaji hao hawa kupaswa kulipa kodi hiyo kwa sababu bado wana msamaha wa kutolipa kodi hadi mwaka 2023 na wengine 2025.

Aidha kwa upande wa mradi wa machinjio ya kisasa alisema upo kwenye hatua ya ukamilishwaji, pamoja na dampo la kisasa ambalo wanazungushia ukuta  na miradi  yote hiyo itakamilika machi mwaka huu, na kubainisha suala la mazingira center limekosa mtu wa kuliendeleza ambapo hivi karibuni watatangaza zabuni tena.

Habari Kubwa