Mbunge awatahadharisha wakulima kuuza chakula

19Feb 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Mbunge awatahadharisha wakulima kuuza chakula

Mbunge wa Vitimaalumu mkoani Shinyanga, Azza Hilali, amewatahadharisha wakulima mkoani humo kutokuuza vyakula hovyo, bali watumie kwa matumizi sahihi ili kukabiliana na tatizo la njaa.

Mbunge wa vitimaalum mkoani Shinyanga, Azza Hilali akitoa salamu kwenye mkutano wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Shinyanga.

Hilali alibainisha hayo jana wakati akitoa salamu kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga kabla ya kuhairishwa, ambao ulikuwa na lengo la kusoma taarifa za utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Alisema mwaka huu kumekuwa na neema ya mvua za kutosha pamoja na wakulima kulima chakula kwa wingi, hivyo ni vyema pale watakapovuna watunze vyakula hivyo kwa akiba ya baadae na kuacha kuvitumia kwa matumizi ambayo siyo ya lazima, pamoja na kuviuza hovyo ili kusije tokea tatizo la njaa.

“Ndugu wajumbe wa mkutano huu naomba tushirikiane kwenda kutoa elimu kwa wakulima ya kutunza vyakula kwa ajili ya akiba ya baadae, kwa sababu mwaka huu mvua zimenyesha za kutosha na wakulima wamelima sana, hivyo ni vyema vyakula hivyo vikatunzwa na huwezi kujua mwakani huenda mvua zikagoma,”alisema Hilali.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya CCM Wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye mkutano wa usomaji wa Ilani ya utekelezaji ya uchaguzi ya CCM Wilaya ya Shinyanga..

“Nazungumza haya sababu najua matatizo ya wakulima wetu, wakiwa na vyakula hua wanajisahau na kuviuza hovyo wakisema na mwakani tutalima tu, ambapo akina baba hua wanauza hukohuko shambani, na akina mama nao wakienda kuchota maji wanaweka kwenye vindoo na kuuza vyakula, ni bora tuchukue hatua mapema,”aliongeza.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Edward Ngelela akiahirisha mkutano huo akifafanua kuna taarifa hazikukaa sawa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga, Edward Ngelela, alikazia suala hilo la uuzaji wa vyakula hovyo, na kufafanua kuwa kipindi cha kilimo familia hua zina upendo, lakini kipindi cha mavuno hua kuna ugomvi kutokana na wanaume kuuza vyakula hovyo na kutumia fedha kwa mambo ya anasa.

Pia alisema wamelazimika kuhairisha mkutano huo mkuu, uliokuwa na lengo la usomaji wa taarifa za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi CCM wilaya, kutokana na taarifa kutokuwa sawa, ambapo leo watazipitia na kuziwasilisha kwenye halmashauri kuu ya CCM Mkoa.

Habari Kubwa