Mbunge aanika vikwazo vya elimu nchini

05May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mbunge aanika vikwazo vya elimu nchini

Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Noah Sapatu, ametaja vikwazo vinne katika elimu nchini Tanzania alivyodai kuwa visipotatuliwa vinaweza kujenga Taifa la walionacho na wasionacho.

Ametaja vikwazo hivyo ni lugha ya kufundishia, ukosefu wa chakula, upungufu wa walimu na ukosefu wa elimu ujuzi.

Ameeleza hayo leo Jumatano Mei 5, 2021 bungeni mjini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Sapatu amesema lugha za kufundishia imekuwa kikwazo kwa watoto wanaosoma shule za Serikali kwa sababu akiwa shule ya msingi anafundishwa kwa Kiswahili lakini akienda sekondari hutumia lugha ya kingereza.

“Watoto hawa wanateseka kwa sababu hawajui lugha ya Kiingereza. Hii inaleta utata mkubwa kwa watoto wanachukia shule. Hawaendi kwa sababu hawaelewi wanapofundishwa,” amesema.

Ameitaka Serikali kuangalia suala hilo na kuhoji ushindani uko wapi wakati katika shule binafsi mtoto anaanza kufundishwa Kiingereza tangu chekechea.

“Hapo kuna usawa ama unawatesa kisaikolojia. Ndio maana shule za Serikali wanafunzi wengi wanapata sifuri nyingi lakini binafsi wanafaulu kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Ametaja kikwazo kingine ni ukosefu wa chakula shuleni, akibainisha kuwa watoto wanateseka kwa sababu Serikali inasema elimu bure, wazazi hawawezi kuchangia wakiamini ni bure.

“Serikali iangalie suala hili kwa sababu wanatengeneza Taifa la walionacho na wasio nacho. Wanafunzi wanateseka wanaingia makorongoni, wanapata mimba. Kwanini Serikali isitoe tamko kuhusu suala hili,” amesema.

Amesema kikwazo kingine ni upungufu wa walimu akidai mtoto anakwenda shule lakini hakuna mwalimu wa fizikia, kemia na baiolojia lakini anafanya mtihani wa mwisho wa kumaliza elimu ya msingi au sekondari.

Sepatu ametaka kikwazo cha nne kuwa ni elimu ujuzi ambapo wanafunzi wamekuwa wakizunguka na vyeti kuhangaika kupata ajira.

Habari Kubwa