Mbunge adai wajawazito wanatozwa 150,000/- kujifungua

21Jan 2022
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Mbunge adai wajawazito wanatozwa 150,000/- kujifungua

MBUNGE wa  Viti Maalumu mkoani Shinyanga,  Santiel  Kirumba (CCM),  amelalamikia wajawazito kutozwa  Sh. 150,000 wanapokwenda kujifungua.

Alitoa malalamiko hayo juzi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ya Shinyanga wakati akichangia taarifa ya afya na kwamba kitendo hicho ni kinyume cha maelekezo ya serikali.

Kirumba alisema katika utoaji wa huduma za afya kwa wajawazito mkoani hapa, bado kuna tatizo hususani kwa upande wa huduma za upasuaji.

Mbunge huyo aliongeza kuwa mjamzito bila kutoa Sh. 150,000 hawezi kupewa huduma ya kuzalishwa mtoto.

"Napenda kujua hili suala la kutoza fedha wajawazito Sh. 150,000 ni utaratibu mpya ambao umetolewa na Wizara ya Afya au likoje? alihoji.

"Hivi karibuni mjamzito katika jimbo la Ushetu wilayani Kahama, alipoteza maisha akiwa hospitalini alipofikishwa kwa ajili ya kujifungua. Kwa kuwa hakuwa na hiyo hela, wauguzi waligoma kumzalisha mtoto mpaka alipe,” alisema.

Pia  alisema kuwa si kila mwananchi ana uwezo wa kutoa kiasi hicho cha fedha na kushauri uangaliwe utaratibu wa kumpatia huduma kwanza, ndipo mambo mengi yafuate na si mtu kufia hospitalini kwa kukosa  fedha.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,  Dk, Daniel Mzee, alisema sera ya afya bado haijabadilika na kwamba mjamzito anatakiwa apewe huduma bure ya kujifungua.

Aliahidi kufuatilia suala hilo na kumpatia taarifa zaidi mbunge huyo kuhusu  wajawazito kutozwa Sh.150,000  kwa kuwa inawezekana kuwa watumishi wachache wanafanya mchezo huo ili kuichafua sekta nzima.

Hata hivyo, Dk. Mzee alisema wajawazito huwa wanatozwa fedha kidogo kwa ajili ya kununua uzi wa kumshonea kutokana na mazingira.

Awali akisoma taarifa ya afya ya mkoani huko,  Dk. Mzee  alisema, wameendelea kuboresha huduma za dharura za upasuaji kwa wajawazito.

Alisema kwa sasa kati ya vituo 23 mkoani hapa, 18 vinatoa huduma hiyo lengo likiwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

Kuhusu vifo vya wajawazito vitokanavyo na uzazi, alisema mwaka 2020 kuanzia Januari hadi Septemba vilitokea 32 na mwaka jana vilitokea 31 ikiwa pungufu ya kifo kimoja.

Alitaja sababu ya vifo hivyo kuwa ni wajawazito kuchelewa kwenda kupata  huduma za afya  na wengi wao hufika wakiwa katika hali mbaya, hivyo hupoteza maisha.

 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,  Sophia Mjema, aliwataka watumishi wa afya mkoani hapa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu kwa kutanguliza utu kwanza badala ya fedha.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa Sh. bilioni 17.4  kwa mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kwamba  kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 7.7   zimeelekezwa sekta ya afya.

Habari Kubwa