Mbunge afanya ziara kushtukiza chanzo cha maji

27Nov 2020
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Mbunge afanya ziara kushtukiza chanzo cha maji

MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini (CCM), Abdulaziz Abood, amefanya ziara ya gafla katika vyanzo vya maji Bwawa la Mindu na kushuhudia uharibifu mkubwa unaofanywa na wakulima kutoka mikoa mbalimbali na kina chake kikiwa hatarini kupungua.

Shughuli za uvamizi wa kilimo katika bwawa hilo, zinahatarisha upatikanaji wa maji kwa wakazi zaidi ya 500,000. Uhakika wa asilimia 75 ya maji inapatikana kutoka chanzo hicho.

Akizungumza na wakazi wa kata za Mzinga, Mindu na Luhungo, wanaozunguka vyanzo vya maji yanayochangia ujazo wa bwawa hilo, Mbunge Abood, alisema kilimo hicho kisipodhibitiwa wananchi wa manispaa hiyo watakosa huduma hiyo.

“Rais Dk. John Magufuli ametukumbuka na kutupa mradi mkubwa wa maji, sasa hatuwezi kuyapata bila kutunza vyanzo vya maji ambavyo vinaharibiwa na kilimo, hivyo lazima tuwe mabalozi wazuri wa kutunza vyanzo vya maji tusikubali viharibiwe,” alisema.

Abood alisema amefanya ziara hiyo na kushuhudia kuwa hali si nzuri kutokana na wakulima kuvamia eneo hilo na kufanya shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia maji yanayotokana kwenye bwawa hilo.

Pia, aliwashuhudia baadhi ya wakulima wakiendelea na shughuli za kilimo mchanganyiko.

Akizungumza na wakulima hao, Abood alisema atakaa na wakulima hao ili kuangalia namna ya kusitisha haraka shughuli hizo na kuwatafutia maeneo mengine ili wakaendelee na shughuli zao za kilimo kwa lengo la kulinda bwawa hilo.

Aliahidi kuchangia miche 10,000 ya miti kwa ajili ya kupandwa pembezoni mwa bwawa hilo ikiwa ni kuunga juhudi za kuzuia uharibifu wa mazingira uliotokana na uvamizi wa shughuli za kibinadamu.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MOROWASA), Tamim Katakweba, alisema wamebaini uvamizi wa shughuli za kilimo ndani hifadhi ya bwawa hilo unafanywa na wakulima kutoka mikoa ya Singida, Kigoma, Mwanza na Dar es Salaam.

Alisema mkakati uliopo ni kuendesha zoezi la harambee kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupanda miti kulizunguka bwawa hilo ambalo ni suluhisho la kudumu.

Habari Kubwa