Mbunge aibua tuhuma za rushwa

25Jun 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Mbunge aibua tuhuma za rushwa

MBUNGE wa Viti Maalum, Salome Makamba (Chadema), jana alilitaka Bunge kusitisha shughuli zake na kujadili kuhusu tuhuma za wabunge kuhongwa fedha ili kutopitisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019.

MBUNGE wa Viti Maalum, Salome Makamba.

Makamba alitoa hoja hiyo bungeni jijini Dodoma jana akitumia Kanuni ya 51(iv) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayoeleza kuwa mambo yanayohusu haki za Bunge, yatawasilishwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa kanuni na endapo wakati wa kikao chochote cha Bunge, jambo lolote litazuka ghafla na litaonekana linahusu haki za Bunge, shughuli zitasitishwa kwa madhumuni ya kuwezesha jambo hilo kuwasilishwa na kujadiliwa isipokuwa tu kama wakati huo kura inapigwa.

Akiwasilisha hoja hiyo, mbunge huyo alisema: "Mheshimiwa Naibu Spika (Dk. Tulia Ackson), Mheshimiwa Cecil Mwambe (Mbunge wa Ndanda-Chadema), ameeleza jambo kubwa sana ambalo linahusiana na Bunge lako.

"Wabunge wako tayari kupewa rushwa, ili kushawishi mabadiliko ya sheria ndogo yaliyoletwa katika Bunge lako tukufu yaweze kupitishwa kwa namna ambayo wabunge hao wataona inafaa.

"Mheshimiwa Naibu Spika, jana (Jumapili), Bunge lako liliita wabunge wachache takribani 40 ili kupewa uelewa wa namna sheria zilizopo kwa hati ya dharura zinataka nini, ila kilichotokea na alichokieleza Mheshimiwa Mwambe, ndio kimenishtua zaidi kwa sababu inaonekana wabunge wale wamepewa rushwa...

"Jambo hilo ni aibu kubwa kwa kuwa 'social media' (mitandao ya kijamii) inazungusha habari hiyo kwamba wabunge wamepewa pesa ili kupitisha miswada hiyo."

Makamba aliliambia Bunge kuwa tuhuma za wabunge kuhongwa zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara na anaona ni busara kwa Kiti cha Spika kuchukua hatua na ikiwezekana kuwafikisha mbele ya Kamati ya Maadili wanaoeneza taarifa hizo kama hazina ukweli.

Akitoa mwongozo kwa mbunge huyo, Naibu Spika (Dk. Tulia) alisema ofisi ya Bunge haina taarifa hiyo na hakuna mtu anayepewa idhini ya kuitisha semina bungeni.

"Ukiitisha watu huko kwingine, si mkutano unaohusu Bunge, hivyo hakuna kibali cha Spika cha kuitisha mkutano uliofanyika jana (juzi) na mimi namsikia yeye (Makamba) na ofisi mimi niko hapa, hatuna hiyo taarifa ya kuita mtu yeyote ya kuja kutoa uelewa kuhusu suala hilo.

"Kwa hiyo, kama kilikuwapo ama ilikuwa vipi, chochote kilichoongelewa huko, ofisi haina taarifa," Dk. Tulia alisema.

Kiongozi huyo wa Bunge alisema hakuna haki yoyote ya Bunge katika matukio hayo iliyovunjwa ambayo inaweza kusababisha chombo hicho kiache kufanya shughuli zake na tujadili jambo la dharura.

Jumamosi, asasi za kiraia Tanzania takribani 30 zilikutana na waandishi wa habari jijini Dodoma na kutoa tamko zikitahadharisha kuwa mabadiliko ya sheria yanayotarajiwa kufanywa na Bunge hivi karibuni hayatakuwa na matokeo chanya na yanakwenda kuzikandamiza asasi hizo.

Katika tamko lao, viongozi wa asasi hizo walidai mabadiliko hayo yakipitishwa, hakuna asasi hata moja itakayokuwa salama na huo utakuwa mwisho wa ajira nyingi za Watanzania na serikali kukosa kodi.

Viongozi hao waliishauri serikali itoe walau muda wa miezi sita ili kujadiliana zaidi na wadau kabla ya kupitisha kuwasilisha muswada huo bungeni, huku wakiweka wazi kuwa wamepanga kwenda mahakamani kudai haki waliyoiita ya wanyonge.