Mbunge akoshwa mipango iliyomo bajeti ya serikali

23Jun 2022
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Mbunge akoshwa mipango iliyomo bajeti ya serikali

MBUNGE wa Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, Prof. Patrick Ndakidemi, amesema bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023 imejikita katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Prof. Ndakidemi alisema yako mambo ambayo wabunge walikuwa wakiyapigia kelele bungeni na bajeti iliyopitishwa hivi karibuni imetoa majibu ya moja kwa moja kwa wananchi wa eneo hilo.

Alisema miongoni mwa mambo aliyokuwa akiisisitiza serikali ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Moshi kwa kuwa kwa sasa imetengewa Sh. milioni 500.

“Nimepiga sana kelele juu ya uwapo wa Hospitali ya Wilaya, tunamshukuru Mungu tumepata Sh. milioni 500 na hospitali hiyo, itaanza kujengwa katika Kata ya Mabogini.

Akizungumzia suala la baadhi ya halmashauri kupata hati chafu na zisizoridhisha katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG), alisema huo ni wajibu wa watu wote katika wilaya husika kuwajibika.

“Niwapongeze Mkurugenzi wa Halmashauri Moshi, Mkuu wa Wilaya, watumishi wa halmashauri hiyo, pamoja na baraza la madiwani kwa kupata hati safi kwa miaka sita mfululizo, hii inaonyesha ushirikiano wa hali ya juu na utendaji kazi wa pamoja.

“Naishukuru halmashauri yangu ya Moshi, imepata hati safi kwa miaka sita mfululizo, niwapongeze Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Mkuu wa Wilaya na watumishi wa halmashauri yetu, lakini kwa halmashauri ambazo zimepata hati chafu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, alishaagiza wote waliochangia kupata hati chafu washughulikiwe,”alisema Prof. Ndakidemi.

Akizungumzia suala la kahawa, alisema zao hilo limekuwa likitoa mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa, na kwa sasa limeshuka thamani, lakini bado ni zao la pili linaloiingizia serikali fedha za kigeni likizidiwa na korosho.

Prof. Ndakidemi alisema serikali ikiboresha baadhi ya vitu kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), kuzalisha miche bora ya zao hilo litaendelea kukua na kukuza pato la taifa na kwa wakulima wenyewe.

“Uwezekano wa kahawa kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa ni mkubwa japo kwa sasa limeshuka lakini bado ni zao la pili linaloiingizia serikali fedha za kigeni, endapo serikali itaboresha zaidi zao hili litaendekea kukua,” alisema.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mabogini, akiwamo Mohamed Issa, alisema bajeti hiyo, imeonyesha dira na mwelekeo wa mafanikio kwa wananchi wa hali ya chini, hasa baada ya kuondolewa kwa ada kwa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano na sita.

Habari Kubwa