Mbunge alia miradi hewa ya maji

12Apr 2017
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mbunge alia miradi hewa ya maji

MBUNGE wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota, amehoji ni kwa nini miradi mingi ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini haifanyi kazi ikiwamo iliyoko mkoani Tabora.

Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, Chikota alisema katika ziara yake, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imekuta madudu kwa baadhi ya miradi kwa kuwa pamoja na kwamba imekamilika miradi hiyo haifanyi kazi.

“Mradi wa Kitere haufanyi kazi kama inavyotakiwa na hili si tatizo la huko, miradi mingi ya umwagiliaji haifanyi kazi LAAC ilitembelea Tabora na kukuta hali hiyo, tatizo ni nini?” Alihoji Chikota.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaac Kamwelwe, alisema kwa sasa miradi ya umwagiliaji nchini inafanyiwa mapitio na kilichobainika zilijengwa skimu za umwagiliaji na kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, baadhi hazifanyi kazi.

“Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuna baadhi ya skimu za umwagiliaji zimekuwa zinafanya kazi mara moja kwa mwaka na si mara mbili kutokana na miradi hiyo kutojengewa mabwawa,” alisema Naibu Waziri huyo.

Kamwelwe alisema wataipitia katika mpango kabambe wa mwaka 2012 kuhakikisha miradi hiyo inafanyiwa usanifu ili ifanye kazi na upungufu utafanyiwa kazi.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia, alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima wa Kitere na Mto Ruvuma kuwa na kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo.

Akijibu swali hilo, Kamwelwe alisema mradi huo umeingizwa katika Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ambao hivi sasa unafanyiwa mapitio ili uendane na hali halisi ya sasa.

Aidha alisema katika mwaka wa fedha 2017/18 Wizara hiyo imeyaweka maeneo hayo katika bajeti kwa ajili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kuendeleza maeneo hayo.

Habari Kubwa