Mbunge ataja sababu zinazoimaliza Kariakoo

19Jun 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Mbunge ataja sababu zinazoimaliza Kariakoo

MJADALA umeibuka bungeni kuhusu mazingira ya uendeshaji wa biashara nchini, utitiri wa kodi na tozo zilivyochangia kuua soko la kimataifa la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wabunge waliochangia kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2018 na mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka wa fedha 2019/20 na mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20, wameitaka serikali kuja na mkakati wa kurejesha biashara ya kimataifa katika eneo la Kariakoo.

Mbunge wa Mvomero (CCM), Sadiq Murad ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara, alisema soko la Kariakoo limepotea katika ramani ya biashara, licha ya kuwa Tanzania ilishafanikiwa kuziteka kibiashara nchi za Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na DRC.

“Leo Kariakoo imepotea kwenye mtandao haipo na sababu za kupotea zipo nyingi ikiwamo suala la namna ya kupeleka fedha za kigeni Dubai, China na nchi nyingine. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti tulikwenda Uganda, unafika unawauliza wafanyabiashara wa Uganda, mbona siku hizi hamji kuchukua mzigo? Wanakwambia sasa hivi wa Dar es Salaam wanakuja kwetu, Malawi wanakuja kwetu, Rwanda wanakuja kwetu, haya ndio majibu tuliyopewa.

“Wale bahari hawana, bandari hawana, BoT (Benki Kuu ya Tanzania) tujiulize kuna nini hapo, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) tujiulize kuna nini hapo? Kwa nini tumelipoteza soko la Kariakoo, bidhaa zile zilikuwa zinapatikana pale zina grade zake (viwango), ukinunua mzigo kule Dubai, China kuna light weight, kuna heavy weight, sasa zile biashara zilizokuwa zinafanyika, TRA hawajui light, hawajui heavy, hawajui nini, wao ni kodi kodi tu, matokeo yake tumeua mtandao wa biashara.”

Sadiq alisema huko ni kuwakatisha tamaa wafanyabiashara, wakati ambao Tanzania ilitakiwa kufungua milango ya Kariakoo.

“Dk. Mpango tusaidiane, tukae pamoja, tuzungumze hili, tuna ushahidi, tuna nia ya kusaidia eneo hii lirudi katika mtandao wa biashara katika nchi zote za maziwa makuu ambazo zimetuzunguka,” alieleza Sadiq.

Sadiq alisema unapokwenda kununua mzigo Dubai au China, ukinunua mzigo wa dola 100,000 wafanyabiashara wa huko wanataka fedha taslimu.

“Je, utaratibu wa kupeleka dola 100,000 ukoje?” Alihoji na kuongeza kuwa ni lazima BoT wasaidie namna bora ya kuhakikisha biashara zinarudi.

“TRA kuna utaratibu ambao unasababisha wafanyabiashara na Watanzania wapate shida, shida namba moja ni zile fomu za usajili, fomu zile zimeandikwa kwa Kiingereza,” alisema na kuongeza:

“Wafanyabiashara wanapata shida kuzijaza, fomu zile zina urasimu, matokeo yake kuna vishoka wamekaa nje kwenye ofisi za TRA wanachukua zile fomu wanawajazia watu, na vishoka wale wanawatoza Watanzania Sh. 10,000 hadi 20,000.”

BASHE AMPA NENO MPANGO

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alimuomba Waziri Mpango akae na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Basgungwa, wafanye mabadiliko makubwa ili kunusuru biashara.

Bashe amemshauri Waziri Mpango kuichukua sheria iliyoanzisha Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na kuziunganisha taasisi zote hizi ndani yake na kisha serikali ianzishe Mamlaka ya Udhibiti Usajili wa Leseni za Biashara ili mtu anapoingia kusajili biashara na kuchukua leseni anapokutana na kila kitu mule ndani, akitoka aende kufanya biashara yake.

NAPE ALIA NA TOZO

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, alisema uamuzi wa kufuta tozo 54 utasaidia kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini, lakini bado kuna tozo nyingine zinapaswa kuangaliwa.

"Pamoja na kufuta tozo ya visima sasa fikirieni kufuta kodi kwenye mitambo ya kuchimba visima vya maji. Mitambo hii itasaidia kuchimba visima pamoja na malango kwa ajili ya umwagiliaji.

"Pia naunga mkono pendekezo la kamati ya bunge kuhusu sekta inayogusa watu wengi ambayo ni kilimo. Ikiguswa inagusa maisha ya watu wengi na ingeweza kupambana dhidi ya umaskini kwa wananchi," alisema.

Vilevile, aliishauri serikali kuongeza wigo wa walipakodi ambao watasaidia serikali kukusanya mapato yakutosha.

SILINDE ATAKA PPP

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde, aliitaka serikali kutambua kuwa maendeleo ya nchi hayategemei kukusanya kodi.

Alisema maendeleo hutegemea kuboresha uwekezaji wa moja kwa moja na ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP).

“Duniani kote maendeleo ya nchi hayategemei kodi pekee, nasema hivi kwa sababu wimbo humu ndani (bungeni) ni kodi tu. Nchi nyingi hutumia kodi kwa matumizi mengineyo na kulipa mishahara,” ameeleza.

Alisema katika Bajeti ya Wizara ya Fedha imeainishwa miradi isiyotekelezeka na kutoa mfano wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambao hivi karibuni Rais John Magufuli alisema mwekezaji alikuwa na masharti magumu.

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, alisema wafanyabiashara hususan wadogo wanakabiliwa na tatizo kwenye mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD).

"Mashine za EFD zimekuwa kero, sijajua tatizo ni kampuni zilizopewa tenda au la. Kila siku ni mbovu sasa zimekuwa mtaji kwa watu utaambiwa mashine mbovu nunua nyingine," 

Naye Mbunge wa Ukerewe (CCM), Joseph Mukundi, alisema uchumi unaonyesha kupanda kwa asilimia saba ambazo zilizotokana na sekta mbalimbali za kiuchumi zilizofanya vizuri ikiwamo ya kilimo ambayo imekuwa kwa asilimia 5.3.Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Ruth Mollel, alisema watumishi wamesahaulika katika maslahi yao hususan nyongeza ya mshahara.

"Nazidi kusisitiza watumishi wa umma ndio walipakodi wazuri anapopokea mshahara, analipa kodi bila kukwepa. Nimeangalia bajeti imetengwa kama Sh. trilioni saba kwa ajili ya mishahara ikionyesha hakuna nyongeza.”

Habari Kubwa