Mbunge ataka DAWASA kutoa elimu kwa "House Girl" matumizi ya maji

04Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbunge ataka DAWASA kutoa elimu kwa "House Girl" matumizi ya maji

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bona Kamoli ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) Kutoa elimu kwa wananchi na wasaidizi wa kazi wa nyumbani (house girl) pamoja na watoto jinsi ya kutumia maji ili kudhibiti matumizi mabaya ya maji.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bona Kamoli.

Kamoli ameitoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea banda la DAWASA katika maonyesho ya kimataifa ya biashara ya 43 maarufu Saba Saba katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es salaam.

Kauli hiyo imekuja kukiwa na malalamiko ya ankara kutoka kwa baadhi ya wateja wa DAWASA ambao wanashindwa kufahamu matumizi yao ya maji kwa mwezi ambapo upelekea usumbufu wakati maafisa wa mamlaka hiyo wanaposoma mita za maji.

Ameipongeza DAWASA kwa kuweza kupeleka huduma ya majisafi kwenye maeneo mengi hususani kwenye yale ambayo hayakuwa na mtandao wa maji kwa muda mrefu.

"DAWASA wamejitahidi kufikisha maji ndani ya Jimbo la Segerea ingawa kuna changamoto sehemu nyingine  maji bado hayapatikani," amesema Kamoli

Amesema kuwa hivi sasa jitihada kubwa zinafanywa na DAWASA kubadili miundo mbinu ya maji iliyokuwa chakavu na kufanikisha kupatikana kwa maji ndani ya Jimbo la Segerea na viunga vyake.

Kwa upande wake Mhandisi wa Uendeshaji na Matengenezo Mkoa wa Tabata DAWASA, Mhandisi Gibson Baragula amemshukuru Mbunge huyo kwa kuona kazi inayofanywa  ya kupeleka maji sehemu zote za Mkoa wa Dar es salaam. 

Amesema kuwa kwasasa wanatoa maji kutoka bomba la Kimara kwenda hadi Bonyokwa na matarajio ni kuhudumia wateja zaidi ya 3,000 ambapo kwa hivi sasa wameshawaunganishia wateja 1400 na wateja 300 wameshafanya maombi ya maunganisho mapya na hivi karibuni wataanza kuwaunganishia.

Habari Kubwa