Mbunge ataka sakafu ya darasa kubomolewa

05Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
HANDENI
Nipashe
Mbunge ataka sakafu ya darasa kubomolewa

MBUNGE wa Handeni Mjini (CCM), Omari Kigoda, ametoa siku saba kwa Mtendaji wa Kata ya Msasa wilayani humo, Hamza Madebe, kubomoa sakafu iliyowekwa kwenye darasa la Shule ya Msingi Mnazi Mmoja kutokana na kuwa chini ya kiwango.

MBUNGE wa Handeni Mjini (CCM), Omari Kigoda.

Kigoda alitoa agizo hilo juzi kwenye ziara yake ya kikazi ya katika kata hiyo kukagua miradi ya maendeleo na alipofika shuleni hapo, alikuta ujenzi wa darasa lakini sakafu yake ikiwa chini ya kiwango, hivyo kuagiza ivunjwe mara moja.

Kigoda alisema hajaridhishwa na maelezo yaliotolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Said Ngungwini, ambaye alionyesha kutoa majibu yasiyo sahihi katika ujenzi huo wakati yeye ndiye msimamizi tangu kuanza ujenzi.

"Natoa mpaka Januari 7, sakafu hii iwe imevunjwa na wahusika kuchukuliwa hatua. Mkishindwa kufanya hivyo hadi hiyo tarehe nitajua nini cha kufanya maana naona mnafanya kazi kwa mazoea,” alisema.

Aidha, Kigoda aliagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu Kaimu Mtendaji wa Mtaa wa Kwalusonge, Kata ya Msasa, Kolimba Mcheto, kwa kutokusoma mapato na matumizi ya mtaa huo kwa miaka miwili.

Wakazi wa mtaa huo walimwambia mbunge kuwa yako makusanyo mbalimbali yakiwemo machimbo ya mchanga, lakini hawajui mapato yake kwa kutosomewa mapato yanayoingia na kutoka kwa miaka miwili.

Juma Kivumbi, mkazi wa mtaa huo, alisema taarifa wanazotoa viongozi katika makusanyo ya mchanga ni Sh. 3,000 kwa lori wakati si kweli kwa kuwa wanakusanya Sh. 10,000 na hawajaambiwa fedha hizo zinafanyia nini.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Athumani Malunda, alisema atawachukulia hatua wenyeviti wote wa mitaa walioingia madarakani kupitia chama hicho watakaothibitika kufanya kazi kinyume cha utaratibu ikiwamo kuwavua madaraka ili iwe fundisho kwa wengine.

Alisema hawawezi kuwavumilia viongozi ambao wanakiuka utaratibu kwa kuwanyanyasa na kuwaibia wananchi badala ya kuwahudumia kitu ambacho ni aibu kwa chama chake.

Habari Kubwa