Mbunge ataka sheria ya habari ifumuliwe

21May 2022
Romana Mallya
DODOMA
Nipashe
Mbunge ataka sheria ya habari ifumuliwe

MBUNGE wa Viti Maalum, Ester Bulaya, jana alishikilia shilingi ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, bungeni akiwatetea waandishi wa habari kwa kutaka Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016 irekebishwe.

Hoja kubwa ya mbunge huyo ni kwamba kundi hilo kwenye baadhi ya maeneo bado linatishiwa na halifanyi kazi kwa uhuru.

Hata hivyo, Waziri Nape aliwaahidi waandishi wa habari kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 mabadiliko hayo yanakwenda kufanyika na tayari mchakato umeshaanza.

HALI ILIVYOKUWA

Mbunge Bulaya wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/23 iliyoomba kupitishiwa Sh. bilioni 282.5, alisema anataka sheria hiyo inapaswa kurekebishwa ili waandishi wa habari walikosoe taifa kwa maslahi ya kujenga nchi.

"Niseme wazi mimi ni mwandishi wa habari na nitawasemea wanahabari. Matatizo  yao nayajua na nimeyaishi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kurudi kwake (wizarani) kaka yangu kuna nafuu, watu wamepata matumaini waandishi wenzangu.

"Na kwa kauli ya Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) imetoa matumaini kwa ile kuonyesha dhamira. Tunahitaji dhamira yako na dhamira ya Rais sasa ije kwenye vitendo kwa kuleta mabadiliko ya Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016,” alisema.

“Mheshimiwa Waziri unajua mbali ya kwamba kuna unafuu lakini bado kwenye maeneo mengine waandishi wa habari wanatishwa, bado waandishi hawafanyi kazi kwa uhuru, Mheshimiwa Waziri unajua leo hakuna stori za uchunguzi kwenye magazeti wala media za kielektroniki," aliongeza.

Bulaya alisema hata makala zinazoandikwa kwa sasa ni za kawaida na kueleza kuwa sheria hiyo ikiletwa bungeni kutakuwa na mijadala ya kujenga na kukosoa Taifa.

"Tunataka turudi enzi hizo tunataka tuone makala za uchunguzi tuone vipindi mbalimbali kwenye redio na luninga, wachambuzi watakuwa huru kwa maslahi ya Taifa, haya yote hayawezi kutokea kama hakutakuwa na sheria bora ya kuwafanya waandishi wa habari wafanye kazi kwa uhuru, kufanya kazi kwa uhuru, kukiwa na uwazi Taifa letu linasonga," alisema Bulaya.

Mbunge huyo alisema lakini leo Rais Samia anaweza kumaliza muda wake na ana dhamira njema pamoja na waziri lakini wakaja wengine wasiokuwa na nia njema wakarudi kule kule kwa waandishi kuteswa, kupigwa, kunyanyaswa, kunyimwa habari kwa maslahi ya Watanzania.

"Niombe Mheshimiwa Waziri ninajua umeanza kukutana na wadau wa habari ni jambo jema lakini ninaomba zile sheria zenye ukakasi serikali mzichukie mzibadilishe kwa sababu ndiyo zinawanyima fursa waandishi wa habari.

"Kwa mfano Mheshimiwa Waziri unajua natolea tu mfano kwenye Sheria ya Huduma ya Habari kifungu cha 19,20,21 ambacho kinazungumzia kinawatambua watu gani ndiyo waandishi wa habari lakini kwenye taaluma yetu tunahitaji wanasheria, madaktari na wachumi wataandika habari kulingana na taaluma zao, lakini kwa sheria hii inataka mtu mwenye shahada ya sheria akija aanze tena kusoma habari, hapana." Alisema Bulaya na kuongeza:

"Tuna Jenerali Ulimwengu ni mwanasheria na ni mwandishi nguli, tuna (Absolum) Kibanda ni mwalimu lakini ni waandishi wazuri, tunahitaji watu wa namna hii kuja kufanya uchambuzi wa kina kwenye tasnia yetu,” alisema Bulaya na kuongeza:

“Lakini watapewa miongozo inayohusu habari, kuna kifungu cha tano(e)(8)(9) kinazungumzia masuala ya leseni kinatoa mwanya mawaziri wenye nia mbaya kufungia vyombo vya habari, ni kifungu kibaya kuliko vyote. Tunaomba vifanyiwe kazi gazeti linatakiwa kusajiliwa tu lakini kila mwaka leseni, hiki kifungu kinatengeneza mazingira ya kufungia vyombo vya habari,” alisema.

Bulaya aliongeza: "Sasa mzigo mzito kapewa Mnyamwezi wakati hii sheria mbovu inatungwa ulikuwapo na unaiona, mzigo unao mwenyewe kipindi kile kilikuwa kingine hiki ni kingine rekebisha hii sheria ili waandishi wa habari tunataka tuwe huru tulikosoe Taifa letu kwa maslahi ya kujenga ili nchi yetu iende kama nchi nyingine.”

AKIJIBU HOJA

Waziri Nape alisema amesikia mchango wa Bulaya na kuwaahidi waandishi wa habari kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 watakamilisha mabadiliko ya sheria hiyo na tayari mchakato umeshaanza.

"Niwaambie nia ya dhati ipo tutafanya mabadiliko na tutasonga mbele kwa pamoja, niwathibitishie zipo sheria mmezitaja mfano Sheria ya Kulinda Takwimu, Sheria ya TEHAMA na nyingine maelekezo ya Rais Samia amesema tupitie sera, sheria, kanuni tuone namna ambavyo zile zilizopitwa na wakati tuzitengeneze na kuzirekebisha,” alisema Nape na kuongeza:

“Ninaahidi wizara yangu sheria zote sera, kanuni tutawashirikisha vya kutosha wadau ili tutunge sheria zinazotokana na mawazo ya watu."

Habari Kubwa