Mbunge ataka uzazi wa mpango kwa wanaume

13Nov 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mbunge ataka uzazi wa mpango kwa wanaume

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Khadija Nassir, ameitaka serikali kuanzisha programu za uzazi wa mpango kwa wanaume kwa kuwa utafiti mbalimbali unaonyesha wana uwezo wa kuwapa mimba wanawake tisa kwa siku moja.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Faustine Ndugulile, picha mtandao

Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Mbunge huyo alisema utafiti mbalimbali duniani unaonesha kwamba mwanaume mmoja ana uwezo wa kuwapa mimba wanawake tisa kwa siku moja, wakati mwanamke mmoja ana uwezo wa kushika mimba moja kwa miezi tisa.

“Je, serikali haioni sasa kuendelea na program za uzazi wa mpango ni uharibifu wa rasilimali badala yake programu za uzazi wa mpango zifanyike kwa akina baba?”alihoji.

Akijibu, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Faustine Ndugulile, alisema ni dhana potofu kwamba uzazi wa mpango ni wanawake peke yao.

“Suala la uzazi wa mpango linawahusu wanaume vile vile na sisi kama serikali tunahamasisha kinababa na mama kushiriki kwenye uzazi wa mpango salama,” alisema.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Zubeda Sakuru, alihoji serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wakunga wa jadi ili kupunguza vifo vya mama na mtoto hasa maeneo ya vijijini.

Akijibu, Dk. Ndugulile alisema Tanzania iliridhia mkataba wa Uzazi Salama mwaka 1994, katika mkutano uliofanyika Misri.

“Mkataba huo unaelekeza kwamba kila mama anayejifungua atahudumiwa na mtaalamu mwenye ujuzi, kwa kutilia maanani kwamba matatizo yatokanayo na uzazi hayatabiriki na yakitokea uhitaji kutatuliwa na wataalamu wenye ujuzi katika kuokoa maisha na mama na mtoto mchanga,” alisema.

Alieleza kuwa Wizara inawatambua wakunga wa jadi kama watu muhimu katika jamii, hivyo Wizara kwa kutambua umaarufu wao katika jamii, inawatumia kufanya uhamasishaji wa wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma na ikibidi kuwasindikiza.

Habari Kubwa