Mbunge ataka wafanyabiashara wa mifugo kufuata taratibu

09Oct 2019
Zanura Mollel
Nipashe
Mbunge ataka wafanyabiashara wa mifugo kufuata taratibu

MBUNGE wa Longido Mkaoni Arusha Dr. Steven Kiruswa amewataka wafanyabiashara wa mifugo kufuata taratibu zilizoweka na serikali hadi hapo meza ya maridhiano baina ya nchi ya Kenya na Tanzania yatakapofanyika juu ya manyanyaso wanayoyapata nchini Kenya.

Ng'ombe.

"Subirini Oktoba 15 tunakutana na viongozi wa Kenya tutapata muhafaka juu ya kero na mateso mnayoyapata mkipeleka mifugo Kenya" alisema Dr Kiruswa

Akizungumza na wafanyabiashara hao ,katika soko la kimataifa la  mifugo lililopo kata ya Kimokouwa kijiji cha Eworendeke, wakati akijibu maswali ya wafanyabiashara hao, alisema hawezi kukinzana na maamuzi ya serikali juu ya kukataza wafanyabiashara watanzania kupeleka mifugo Kenya.

"Mnahitaji changamoto zenu zitatuliwe, subirini serikali zikutane,ila siwezi kusema mpeleke mifugo Kenya wakati hali yenu ya kiusalama mnadai ni ndogo" alisema Dr Kiruswa

Aidha aliwaeleza kuwa ,kumekuwa na tabia ya baadhi yenu kutumia maamuzi haya ya kuzuiwa kupeleka mifugo Kenya kupita njia zisizo rasmi ( Panya), na kuwataka kuacha mara moja tabia hiyo kwani huko nikupotezea nchi mapato na kuonekana hakuna misimamo katika maamuzi ya serikali.

"Mpaka umemwaga maaskari wakutosha kuanzia wilaya ya Rombo hadi hapa Longido, mtakamatwa na hatua mtachukuliwa,tiini mamlaka ya serikali" aliwataka Dr Kiruswa

Akizungumzia kuwepo kwa malalamiko ya Passport za Single Journey, alisema alishawasilisha taarifa kwa mamlaka husika ambayo ni  Ofisi ya Uhamiaji Wilaya kusogeza huduma ya upatikanaji wa passport kubwa ili kurahisisha shughuli za kibiashara .

Alifafanua kuwa, ili uweze kupata passport kubwa ni lazima uwe na kitambulisho cha Taifa, hivyo aliwataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanajisajili mamlaka ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili waweze kusaidika kwa wakati.

"Mnaweza kuomba passport ya jumuiya ya Afrika mashariki rangi yake ni ya blue, hutumika kwa miaka mitatu, ili upate passport hiyo unatakiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa, barua kutoka kwa mtendaji inayothibitisha taarifa zako pamoja na leseni ya udereva gari au pikipiki" alifafanua Dr Kiruswa.

Dr Kiruswa alisema , kuhusu tozo mliyoiomba serikali kuwapunguzia, aliwasihi kuendelea kutii sheria za nchi, hadi hapo wizara husika itakapo tatua kero hiyo, lakini pia kiwanda cha kuchakata nyama cha Elias food overseas kilichopo kijiji cha Eworendeke kitakapo kamilika kero ya tozo mnayoilalamikia itakua imetatulika.

"Hii ni vita ya kibiashara baina ya Kenya na Tanzania, mnalalamika kuteswa mkienda Kenya bado mnataka tena kwenda kabla maamuzi ya meza moja hayajatolewa, haiwezekani, mifugo iliyopo hapa angalieni utaratibu mwingine kama mtarudisha nyumbani au kusubiri mazungumzo" alisema Dr Kiruswa.

Shabani Ibele mkazi wa Singida ambaye pia ni mfanyabiashara wa mifugo, alisema hawana uhuru wa makubaliano ya biashara hususani katika magari ya kupakia mifugo kwenda Kenya, wananyimwa kuingia na magari yao ya Tanzania.

"Nasikitika sana kuona wakenya wakija kununua vitunguu nchini Tanzania wanaingia hadi mashambani tena na magari yao, lakini sisi tunanyimwa kuingia na ya kwetu magari yetu mwisho ni hapa sokoni, tunashusha yanapakiwa na magari ya Kenya alafu tunalipia yale magari tena" alieleza Ibele.

Mbardada Ole Mbaridi mkazi wa Monduli alidai baadhi ya wafanyabiashara hawajapata taarifa juu ya kuzuiwa kwa mifugo kwenda Kenya, hivyo kupeleka wafanyabiashara wengine kuendelea kuleta mifugo sokoni na hakuna suluhu ya kupeleka Kenya.

"Mifugo ipo hapa, hatujui tufanyaje hatukupata taarifa kama hali si shwari, serikali tunaomba itusaidie" aliomba Mbaridi.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mifugo soko hilo Saruni Laizer alisema wafanyabiashara wanataarifa lakini wengine wanaonekana kuwa wakaidi kuhusiana na maamuzi yaliyotolewa na serikali.

"Minada yote inaviongozi ambao ni wenyeviti, taarifa wanazo na niliwaambia wawaeleze wafanyabiashara kusitisha biashara ya mifugo hadi hali itakapo kuwa shwari" alisema Saruni.

Kwa upande wake afisa tawala wilayani hapa Malaki Tate alisema msimamo wa serikali utabaki palepele hadi suluhu itakapo patikana, waacheni waje kununua mifugo hapa ila ninyi ni marufuku kupeleka Kenya.

"Tumezuia kwa ajili ya usalama wenu, hata sasa  tumesikia wanakuja wenyewe kufuata mifugo hapa, waacheni waje hata hizi tozo mnazolalamika kuwa kubwa watalipa wao ikiwa ni sh 9,000 na 30,000, hadi zile za Kenya mnazosema natozwa watalipa wao" alielez Malaki

Habari Kubwa