Mbunge CCM aitaka serikali ihalalishe kilimo cha bangi

21May 2019
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe
Mbunge CCM aitaka serikali ihalalishe kilimo cha bangi

WAKATI Jeshi la Polisi likipiga vita kilimo cha bangi na kuharibu mashamba yaliyolimwa kilevi hicho, Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM), ameishauri serikali kuruhusu kilimo cha bangi kwa ajili ya utengenezaji wa dawa za binadamu.

Akichangia mjadala bungeni jijini Dodoma jana kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka ujao wa fedha, Kishimba alisema nchi tayari nne barani Afrika zimeruhusu kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya dawa za binadamu.

"Ni vizuri kama dunia inapopata kitu kizuri ni vyema Watanzania tukawahi. Ninavyoongea kuna gazeti... (alitaja jina la gazeti) la tarehe 15 limesema Uganda imesharuhusu kulima bangi kwa ajili ya dawa za binadamu," Kishimba alisema.

Mbunge huyo aliongeza kuwa asilimia 80 ya dawa za maumivu ya saratani zinatokana na bangi.

"Nashangaa wataalamu wetu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), wangekuwa wameshachukua sampuli na wangewajulisha kuwa dawa zilizo na bangi ndani yake.

"Wangemuuliza msambazaji hiyo bangi anaitoa wapi? Mheshimiwa Spika, sisi wenyewe tunayo bangi hiyo, tunaona kila siku inakatwa, ukweli nyingi siyo kwa ajili ya kuvuta. Bangi hiyo imekuwa ikienda katika dawa za binadamu," Kishimba alisema.

Aliendelea kujenga hoja yake akieleza kuwa mbali na Uganda, nchi za Lesotho na Zimbabwe pia zimeruhusu kilimo cha bangi na kuna viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu kwa kutumia bangi.

Alilieleza Bunge kuwa gunia moja la bangi nchini linanunuliwa kwa bei ya kati ya Sh. milioni nne na Sh. milioni 4.5 na kwa Lesotho na Zimbabwe, gunia moja linauzwa Sh. milioni 20.

"Bangi karibu yote ya Tanzania inakwenda katika dawa za binadamu ambazo tunaletewa kutumia. Kuna ubaya gani (nchi) ikaanza kutoa vibali kwenye maeneo mbalimbali na kuhalalisha watu waanze kulima bangi hiyo na kupata faida?" Kishimba alihoji.

Mbunge huyo alisema haungi mkono kauli ya Mbunge wa Geita, Joseph Musukuma (CCM), ambaye amekuwa akitaka bangi kuhalalishwa kwa ajili ya kuvuta.

"Ni vizuri Waziri wa Kilimo (Japhet Hasunga) awasiliane na Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu) waone namna gani watafanya, lakini watambue kwamba bangi ni zao ambalo pia haliliwi na wadudu. Hekari moja ya bangi unapata gunia sita," alisema.

Baada ya Kishimba kuwasilisha mchango wake, Spika wa Bunge Job Ndugai, alimpongeza mbunge huyo kwa uwasilishaji mzuri na kuwataka wabunge kuiga uchangiaji wa kujikita katika eneo moja.

"Niwape siri, muongee kama Kishimba, unakuja na kitu chako fulani, unajikita sehemu moja. Hii hoja ni nzuri sana, naamini Jenista (Mhagama - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Watu Wenye Ulemavu) ameipigia mstari," Spika Ndugai alisifu.