Mbunge CCM alia na tozo za trafiki

16May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
The Guardian
Mbunge CCM alia na tozo za trafiki

MBUNGE wa Ulanga Mashariki, Godluck Mlinga (CCM), ametahadharisha kutokea kwa mgomo wa madereva wa mabasi nchi nzima kutokana na kile alichokiita uonevu dhidi yao unaofanywa na Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za serikali.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali' bungeni jijini Dodoma jana, Mlinga alisimama na kuomba kuahirisha shughuli za Bunge za jana ili kujadili hoja hiyo ya dharura.

"Mheshimiwa Naibu Spika, nasimama kwa Kanuni ya 47 inayotaka kusitisha shughuli za Bunge na kujadili hoja ya dharura.

 

Hivi ninavyoongea, kuna mgomo baridi wa madereva wa mabasi kote nchini ukianzia Morogoro.

"Kwanini madereva wa mabasi wanataka kugoma? Sasa hivi, kwenye mabasi yote kumefungwa ving'amuzi vya VTS na kudhibitiwa na Sumatra na wakizidisha 'speed' 85, wanapata alama moja kwa kila tendo la kuzidisha."Kwa mfano kutoka Morogoro hadi Dar es Saalaam kuna umbali wa kilometa 193.

 

Kuna vibao vya 50 vinavyozidi 22. Kuna zebra zinazozidi 22. Ukifuata taratibu zote kutoka Dar es Salaam, kufika Morogoro utatumia muda wa saa sita.

"Mheshimiwa Naibu Spika, ukizidisha 'speed' 50, unapigwa faini na trafiki. Usiposimama kwenye zebra, unapigwa faini na trafiki.

 

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tendo moja la kuzidisha 'speed' 85 unapopewa alama, jumla ya alama utakazopata kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam unaweza kupigwa faini kati ya Sh. milioni mbili hadi tatu kwa safari moja.

"Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni wizi, uonevu, tunataka kwenda kwenye nchi yenye uchumi wa kati lakini kwa mwendo huu hatuwezi kufika.

 

Kutokana na hilo, naomba shughuli za Bunge ziahirishwe tujadili hoja hii. Naomba kutoa hoja," Mlinga aliwasilisha.

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa anaongoza kikao, alikataa kuahirisha shughuli za jana za Bunge kujadili hoja hiyo lakini akaitaka Serikali kukaa na pande zinazohusika kutatua changamoto zinazolalamikiwa na madereva.

"Kanuni ya 47 inafanya kazi pamoja na Kanuni ya 48. Kwa maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Mlinga na kwa mujibu wa Kanuni ya 47(4) na Kanuni ya 48(4), jambo hili linaweza kushughulikiwa katika utaratibu wa kawaida.

"Na kwa sababu baadhi yetu tumelisikia hapa na serikali ipo hapa bungeni, ichukue hatua kuona ni mambo gani ambayo yanalalamikiwa na madereva ili nchi iweze kuendelea wakati huo huo kama waheshimiwa wabunge tukijitahadharisha na ajali zinazotokea.

 

"Kwa hiyo, upande wa serikali wakutane na hawa madereva kuona shida iko wapi na wamiliki wa vyombo ili wote tuweze kwenda kwa pamoja wakati huo huo wajibu wa serikali kutulinda dhidi ya ajali upo palepale," Dk Tulia aliagiza.