Mbunge matatani madai ya rushwa

10Jul 2020
Joctan Ngelly
Kigoma
Nipashe
Mbunge matatani madai ya rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma imemkamata aliyekuwa Mbunge wa Buhigwe, Albert Ntabaliba, maarufu kama Obama, kwa tuhuma za rushwa.

Sambamba na Obama, kiongozi mwingine aliyekamatwa ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Buhigwe, Everina Muhungo. Wawili hao wanadaiwa kugawa fedha kwa wajumbe waliohudhuria kikao cha ndani kilichofanyika Julai 7, mwaka huu, katika Kata ya Mnanila wilayani humo.

Maofisa wa Takukuru waliokuchua fedha hizo zinazokadiriwa kuwa zaidi ya Sh. milioni 2.2 zilizokuwa zimepangwa kuwagawia wajumbe katika kikao hicho.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Stephen Mafipa, alisema Julai 6, mwaka huu, walipokea simu kutoka kwa wasiri wao kuwa Obama alikuwa akifanya vikao vya ndani kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kata mbalimbali wilayani humo.

Mafipa alisema vikao hivyo vilikuwa vikiambatana na utoaji wa fedha kwa wajumbe ambao alikuwa akikutana nao na kwamba kiwango cha fedha ambacho kilikuwa kikitolewa ni kulingana na idadi ya wajumbe.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, walifanya ufuatiliaji kwa kuwasiliana na CCM Wilaya na kuelezwa kuwa vikao anavyovifanya ni halali lakini kama kuna kitu kingine kinatokana na vikao hivyo ambacho ni vitu vya thamani si halali.

Baada ya hapo, alisema Julai 7 aliwatuma maofisa wake kwenda Buhigwe kufuatilia vikao anavyovifanya ambavyo kwa mujibu wa taarifa vilikuwa vimalizike jana.

Kwa mujibu wa Mafipa, maofisa wa TAKUKURU baada ya kwenda kufatilia vikao hivyo, walipenya na kuingia katika kikao ambacho kilikuwa kikifanyika katika Kata ya Mnanila majira ya saa 8:00 mchana.

Alisema baada ya kikao kumalizika, Muhungo alionekana akigawa fedha Sh. 10,000 kwa kila mjumbe na wakati huo anakamatwa alikuwa ameshagawa Sh. 210,000 kwa wajumbe.

Wakati anagawa fedha hizo, Mafipa alisema maofisa wa TAKUKURU waliingilia kati na kuzuia shughuli hiyo na kuamuru wajumbe wote ambao walikuwa wameshapokea fedha hizo, warudishe na Sh. 210,000 zilisalimishwa mbele ya maofisa wa TAKUKURU waliokuwapo kwenye kikao hicho.

Pia alisema maofisa wa TAKUKURU walimtaka Obama kusalimisha fedha zote alizokuwa nazo eneo hilo la kikao na kukabidhi Sh. Milioni mbili alizokuwa nazo.

Mafipa alisema fedha zote ziko katika ofisi za TAKUKURU mkoa wa Kigoma na upelelezi wa tukio hilo unaendelea na baada kumalizika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Pamoja na kukamata fedha hizo na kumtia mbaroni, Mafipa alisema taasisi yake ilimruhusu Obama kuendelea na vikao vyake kwa mujibu wa ratiba huku akitahadharishwa kutoendelea kugawa fedha.

Hata hivyo, Mafipa alisema baada ya kukamatwa, watuhumiwa hao walidai kuwa kikao kilitakiwa kianze majira ya saa 3:00 asubuhi, ndiyo maana aliwagawia fedha wajumbe hao kwa ajili ya chai.

Alisema baada ya kuchukuliwa maelezo ya awali, Muhungo alikiri kuwa Obama ndiye aliyempatia fedha hizo ili awagawie wajumbe baada ya kikao kumalizika.

Habari Kubwa