Mbunge mwingine Chadema mbaroni

03Aug 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbunge mwingine Chadema mbaroni

MBUNGE wa Momba kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Pascal Haonga, amekamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu katika kituo cha Vwawa Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe.

MBUNGE wa Momba kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Pascal Haonga.

Kwa mujibu wa msaidizi wa Haonga, Mwalusanya Wilfred, mbunge huyo alikamatwa jana mchana na kisha kuhojiwa kwa muda kabla ya kuwekwa kwenye mahabusu hiyo.

Alisema Mbunge huyo anashutumiwa na Jeshi la Polisi kuwa ndiye aliyehamasisha mgomo wa madereva wa malori yanayofanya
safari zake kati ya Mbozi na Tunduma.

“Hiyo njia ni mbovu," alisema Wilfred na "kwa muda mrefu wenye malori wamelalamika, lakini hakuna hatua ambazo zinachukuliwa."

"Sasa wameona wagome ndipo polisi wakadhani kuwa Mbunge ndiye amehamasisha mgomo.”

Alisema Mbunge huyo alihojiwa peke yake bila kuwa na mwanasheria yeyote na walipohoji makosa yake waliambiwa kuwa wanasubiri maelekezo kutoka juu.

“Hivi sasa tuko kwa OC CID na tumemwomba atuambie watamwachia saa ngapi au watampeleka mahakamani muda gani ili tujue cha kufanya, lakini ametujibu kuwa wanasubiri maelekezo kutoka juu,” alisema Wilfred.

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alithibitisha kuweka ndani kwa Mbunge huyo huku akitaja sababu ya kukamatwa kwake kuwa huenda ni mkutano wa hadhara alioufanya juzi.

“Alifanya mkutano jana (juzi) na kuzungumzia adha ya barabara inayotoka Mbozi kwenda Tunduma. Sasa hayo mambo ndiyo yamewakera wakubwa," alisema Makene.

Aidha, Makene alisema anashangaa kuona Mbunge huyo akiwekwa mahabusu kwa muda mrefu wakati alishachukuliwa maelezo yake na kwa hadhi yake angeweza kujidhamini mwenyewe.

“Kosa la uchochezi linadhaminika, na yule ni Mbunge. Kwanini wamweke mahabusu kwa kosa ambalo kisheria linadhaminika?" Alihoji Makene.

"Sisi tunaona huu ni mwendelezo wa kuwakamata na kuwatisha wanachama na viongozi wa chama chetu.”

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange, alisema yuko nje ya ofisi na asubiriwe atakaporejea.

“Nikirudi nitazungumza,” alisema Nyange.

Kuwekwa mahabusu kwa Haonga kunakuja siku chache tangu Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akamatwe na polisi akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Julai 20 akielekea Kigali, Rwanda kwenye mkutano kabla ya kupandishwa mahakamani kwa kosa la uchochezi.

Aidha, Julai 15 Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji, Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe na Mbunge wa Viti Maalum, Zibeda Sakuru na viongozi wengine wa ngazi za chini walikamatwa na Polisi wilayani Nyasa wakati wakiwa kwenye kikao cha ndani.

Habari Kubwa