Mbunge mwingine upinzani matatani

19Mar 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mbunge mwingine upinzani matatani

MBUNGE wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali, ameingia matatani baada ya kudaiwa kumkashfu Spika wa Bunge, Job Ndugai.

MBUNGE wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali, picha mtandao

Ndugai amelalamika kuwa mbunge huyo alimkashfu alipozungumza na waandishi wa habari juzi, hivyo anafikiria hatua stahiki za kumchukulia.

Lijualikali anasubiri adhabu yake kutoka kwa Spika Ndugai kutokana na maelezo aliyoyatoa juzi dhidi ya kiongozi huo wa Bunge yaliyodaiwa kujaa tuhuma na kejeli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Bunge, maelezo yaliyotolewa na mbunge huyo yamesheheni tuhuma zenye kejeli na dharau dhidi ya Spika na ofisi yake.

“Maelezo hayo aliyatoa wakati akizungumza na waandishi wa habari juzi, Spika Ndugai anatafakari hatua za kinidhamu za kumchukulia Lijuakali,” ilisema taarifa hiyo.

Alhamisi iliyopita, Bunge lilitoa taarifa kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Spika Ndugai amemwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, kumwarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki liko wazi.

Taarifa ya Bunge ilibainisha kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki linaloongozwa na Nassari aliyedhaminiwa na (Chadema) liko wazi kutokana na Mbunge huyo kupoteza sifa.

Vilevile taarifa hiyo ilisema Nassari amepoteza sifa hiyo kwa kutohudhuria mfululizo mikutano ambayo ni mkutano wa 12 wa Septemba 4 hadi 14, mwaka 2018, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16 na mkutano mwaka 2018.

Pia taarifa hiyo ilisema Nassari hakuhudhuria mkutano wa 14 uliofanyika kuanzia Januari 29 hadi Februari 9, mwaka huu.

“Uamuzi huu wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71 (1) (c). Ibara hii inaeleza kuwa, ‘Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika,” ilisema.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ibara hiyo imefafanua katika Kanuni ya 146 (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.

“Kanuni hiyo inaeleza kuwa, ‘Kuhudhuria vikao vya Bunge na Kamati zake ni wajibu wa kwanza wa Mbunge, Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano  ya Bunge mitatu mfululizo  bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge  wake na Spika ataiarifu NEC,” ilisema.