Mbunge wa Chadema amwita Waziri Mwigulu gereza la Moshi

08Aug 2016
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Mbunge wa Chadema amwita Waziri Mwigulu gereza la Moshi

MBUNGE wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffary Michael, amemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akimwomba atembelee gereza kuu la Karanga-Moshi, kwa kuwa linakabiliwa na changamoto nyingi, ukiwamo msongamano wa wafungwa na mahabusu kwa asilimia 5.9.

Mkaguzi Maalumu na Mbunge wa Moshi Mjini Jaffary Michael (mwenye skafu shingoni), akiagana na Mkuu wa Gereza Kuu la Karanga-Moshi, Dk. Hassan Mkwiche, baada ya kulikagua na kutoa misaada ya kibinadamu.

Sababu zinazotajwa kusababisha msongamano huo ni kukosekana kwa magereza ya Wilaya ya Hai na Siha, kucheleweshwa kwa upelelezi wa kesi za mauaji, unyang’ang’anyi na tatizo la usafiri kwenda mahakamani na hasa mahakama za mwanzo.

Alikuwa akijibu risala ya Mkuu wa gereza hilo, Dk. Hassan Mkwiche, muda mfupi baada ya kuitembelea juzi na kutoa misaada ya kibinadamu.

“Jumatatu (leo), nitakuwa nimeshamwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu), kumwomba aje gereza kuu la Karanga, kwa sababu mambo mengi yanayohitajika yanahusu Wizara yake. Bado tuna safari ndefu ya kuboresha huduma za magereza.

Nimekuja hapa kuwafariji na kuona naweza kwa kiasi gani kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto,” alisema Jaffary.

Kabla ya majibu hayo, Mkuu wa gereza hilo, Dk. Mkwiche, alimweleza Mbunge huyo kwamba moja ya changamoto kubwa inayowakabili ni msongamano wa mahabusu na wafungwa uliofikia asilimia 5.9.

“Huduma za usafiri za kila siku, tunalo gari aina ya Land Cruiser Pickup ambalo lipo katika hali mbaya sana kwa uchakavu wa tairi kiasi cha kuhatarisha usalama wa watumiaji, tunakuomba uone jinsi ya kutusaidia tairi mpya. Hata hivyo, tunayo kompyuta moja tu, printer (kinakilishi) na mashine ya kudurusu (photocopy mashine)…Tunakuomba navyo utusaidie,” alisema Mkuu wa gereza.

Mbali na vifaa hivyo, imo pia changamoto ya mahitaji makubwa ya karatasi kwa ajili ya kuchapisha kusudio la kukata rufani na masahihisho ya hukumu.

Kufuatia changamoto hizo, mbunge huyo alitoa msaada wa mafuta ya chakula ndoo 10, matairi kwa ajili ya gari hilo, msaada wa karatasi na kuahidi kutafuta wadau watakaosaidia upatikanaji wa kompyuta na jozi yake yote pamoja na watakaojitokeza kutoa misaada ya magodoro, mashuka na mablanketi.

Habari Kubwa