Mchungaji aonya wanawake wanaonyanyasa waume zao

07Mar 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Mchungaji aonya wanawake wanaonyanyasa waume zao

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Julia Celestine, Dayosisi ya Mashariki mwa Ziwa Victoria, Buzuruga jijini Mwanza, amewataka wanawake kuacha matukio ya ukatili nyumbani mwao kwa kunyanyasa wanaume.

Akizungumza jana kwenye siku ya maombi ya wanawake duniani, yaliyofanyika mjini hapa kwenye kanisa la Africa Inland Tanzania (AICT) Ngokolo.

Mchungaji huyo aliwataka wanawake wawe watii katika ndoa zao ili kuepusha vifo vya ghafla kwa waume zao na kubaki wajane.

Alisema baadhi ya wanawake wamegeuka kuwa wanyanyasaji wakubwa kwa waume zao, hasa pale wanapotoa fedha za Vicoba na kujiona kichwa katika familia na kuanza kuwadharau wanaume na hata kuwanyima unyumba.

Celestine alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha wanaume kufariki dunia kwa mshituko wa moyo na msongo wa mawazo kwa sababu ya kuhifadhi mambo hayo moyoni.

Katika hatua nyingine, wanawake mjini Shinyanga wameiomba serikali kutokomeza matukio ya mauaji dhidi yao kwa kukatwa mapanga na kunyofolewa viungo vyao vya siri.

Katibu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Manispaa ya Shinyanga, Tekla Mongela, alisema hayo jana wakati akisoma risala kwenye maombi hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko.

Alisema changamoto kubwa ambayo inawakabili wanawake ni kuwapo matukio ya mauaji ya wanawake na kunyofolewa viungo vyao vya siri, hali ambayo imekuwa ikiwakosesha amani, hivyo kuiomba serikali ikomeshe matukio hayo.

“Tunaiomba serikali itokomeze matukio ya mauaji dhidi ya wanawake pamoja na kutolewa viungo vyetu ili tuishi kwa amani katika nchi yetu kwa sababu mauaji haya yanatunyima amani,” alisema Mongela.

Kwa upande wake, Mboneko alisema serikali itaendelea kuimarisha ulinzi ndani ya jamii pamoja na kuwachukulia hatua waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi na kusababisha mauaji ya watu wasio na hatia.

Mboneko pia aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Habari Kubwa