Mchunguzi TAKUKURU mbaroni tuhuma rushwa

12Sep 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Mchunguzi TAKUKURU mbaroni tuhuma rushwa

OFISA Uchunguzi Mwandamizi (II) wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni, Nina Saibul, amekamatwa na taasisi hiyo kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh. milioni 4.9.

Taarifa iliyotolewa jana na TAKUKURU na kutiwa saini na Ofisa Uhusiano wake wa makao makuu, Doreen Kapwani, ilisema ofisa huyo anadaiwa kuomba rushwa hiyo kutoka kwa mfanyabiashara anayejihusisha na shughuli za ujenzi wa nyumba za kupangisha (Real Estate).

Ilisema kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa taarifa za watuhumiwa wengine, TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni ilipokea taarifa za malalamiko dhidi ya ofisa wake huyo kuomba rushwa ili asiendelee na uchunguzi unaodaiwa kuwa ulikuwa ukiendelea.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa baada ya taarifa hiyo kupokewa uchunguzi wa awali wa kuthibitisha tuhuma hizo ulifanyika na kubaini kuwa upo ukweli wa tuhuma hizo za kuomba hongo, lakini hakukuwa na tuhuma wala jalada lolote la uchunguzi unaoendelea dhidi ya mlalamikaji.

“Baada ya TAKUKURU kujiridhisha na uchunguzi huo wa awali, iliandaa mtego uliowezesha kukamatwa kwa Nina na mumewe, Ramadhani Makoye, wakipokea kiasi hicho cha pesa kilichoombwa na Nina,” ilibainishwa katika taarifa hiyo.

Ilisema taasisi hiyo imechukua hatua hiyo ili kuhakikisha inajisafisha dhidi ya watumishi wake wachache wenye tabia ovu zenye kuchafua taasisi hiyo na kwamba uchunguzi wa shauri hilo unakamilishwa ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani.

“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, tunawashukuru wananchi na wadau wengine ambao wameendelea kushirikiana na taasisi katika kufanikisha jukumu hili la kuzuia na kupambana na rushwa kwa kuleta taarifa," alisema Doreen katika taarifa yake hiyo.

Habari Kubwa