Mdahalo wapaza sauti dhidi ya Sheria Ndoa ya 1971

27Jun 2017
Said Hamdani
LINDI
Nipashe
Mdahalo wapaza sauti dhidi ya Sheria Ndoa ya 1971

WADAU wa maendeleo ya elimu wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, wamesema kukuthiri kwa ndoa za utotoni nchini kunachangiwa na serikali kuruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri mdogo wa chini ya miaka 18.

Walitoa malalamiko hayo walipokuwa wakichangia kuhusu haki zinazohusu mtoto kwenye mdahalo uliofanyika viwanja vya Maalim Seif katika mji mkongwe wa Kivinje.

Salum Abdallah alisema kushamiri kwa ndoa za utotoni nchini kunachangiwa na serikali wa kutobadilisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo imepitwa na wakati.

Salum alisema kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 13 na 17, inatoa uhuru kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri mdogo wa chini ya miaka 181.

Alisema kama katiba ya Tanzania, inaelekeza umri wa mtu mzima wa kujitegemea ni miaka 18 na kuendelea, hivyo ni vema basi Serikali kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili haki za watoto hususani wa kike ziweze kupatikana.

Kindamba Abdallah, alisema licha ya serikali kufikishwa mahakamani na mwanaharakati Rabel Juni na mtangazaji wa kipindi cha Femina kuhusiana na kupinga kipengele hicho na mahakama kumpa ushindi, hakuna jitihada zinazoonyesha utekelezaji wake.

Alisema kama vipengele hivyo havitafanyiwa kazi ni dhahiri ndoa za utotoni zitaendelea kushamiri, huku mtoto wa kike nchini akiendelea kunyimwa zile haki zake za msingi ikiwamo ya kupata elimu.

Hadija Selemani na Pili Kuliwa, walisema watoto wa kike kuolewa wakiwa na umri mdogo, kunachangia changamoto nyingi ikiwamo kujifungua kwa upasuaji.

Mdahalo huo uliandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Tujikwamue wanawake wa Kilwa (Tujiwaki), kwa lengo la kuelimisha wazazi, walezi na jamii kuachana na vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto hasa wa kike.

Habari Kubwa