Mdee aachiwa huru kesi madai ya kumkashifu Rais

26Feb 2021
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mdee aachiwa huru kesi madai ya kumkashifu Rais

MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee, ameachiwa huru baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha tuhuma za kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Mdee aliachiwa huru jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hakimu alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri, bila kuacha shaka umeshindwa kuthibitisha kesi kwa Mdee.

"Jamhuri wana jukumu la kuthibitisha kesi bila kuacha shaka dhidi ya mshtakiwa. Katika kesi hii, ushahidi umeshindwa kuonyesha kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma zinazomkabili, mahakama hii inamwachia huru," alisema hakimu.

Alisema ushahidi wa mashahidi watatu wote askari polisi upande wa Jamhuri, umeshindwa kuthibitisha kuwa Mdee alitoa maneno ya uchochezi, hivyo mahakama imemwona hana hatia.

Hakimu Simba alisema shahidi wa kwanza katika ushahidi wake, alidai kuwa yeye ndiye aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa na maelezo hayo yalikataliwa mahakamani hapo, kwa hiyo ushahidi wake hakuthibitisha kosa alilokuwa akituhumiwa nalo.

Alisema shahidi wa pili katika ushahidi wake, alidai kuwa yeye aliona kwenye mtandao wa kijamii wa ‘YouTube’ mshtakiwa akitoa maneno ya uchochezi, lakini alishindwa kuyathibitisha mahakamani.

Kwa upande wa shahidi watatu, ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, yeye aliambatana na askari mwingine (Inspekta Patrick) kwenda kumkamata Mdee.

Akichambua uamuzi, hakimu alisema shahidi huyo aliagizwa kwenda kumkamata Mdee nyumbani kwa wazazi wake Ubungo, Dar es Salaam, ambako alimkuta mama yake na kumweleza kuwa anataka kumkamata mshtakiwa.

"Ushahidi pekee wa Jamhuri ni huu katika kesi hii unaothibitisha kuwa Mdee alikamatwa na kufunguliwa mashtaka haya," alisema Hakimu Simba. 

Katika utetezi wake, Mdee alidai kuwa anamfahamu Rais wa Tanzania ni John Pombe Joseph Magufuli na hajui kama kumtukana Rais au mtu yeyote ni kosa la jinai. 

Alidai Machi 13, 2017 alikuwa mwanachama wa CHADEMA na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) na kwamba siku hiyo hapakuwapo na mkutano wa chama katika ofisi za makao makuu. 

Mdee alidai kuwa hajui kama kulikuwa na mkutano na waandishi wa habari siku hiyo na hakuna mashahidi waliosema siku hiyo kulikuwa na mkutano huo.

Akihojiwa na wakili wa utetezi Edson Kilatu, Mdee alidai Kinondoni hakuna mahali panapoitwa Ufipani na kwamba Makao Makuu ya CHADEMA yako Mtaa wa Ufipa. 

Mdee anadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mtaa wa Ufipa Manispaa ya Kinondoni, alitenda kosa la  kutoa lugha chafu.

Anadaiwa alitamka maneno machafu dhidi ya  Rais John Magufuli kuwa  “anaongea ovyo ovyo, anatakiwa  afungwe breki”  na kwamba kitendo hicho kingesababisha uvunjifu wa amani. 

Habari Kubwa