Mdee ahimiza kupigania haki za watoto bila hofu

03Sep 2017
Cynthia Mwilolezi
Nipashe Jumapili
Mdee ahimiza kupigania haki za watoto bila hofu

MWENYEKITI wa Taifa wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha),Halima Mdee, amepanda mti kwenye kituo cha kutunza watoto wenye mahitaji maalum cha Samaritan Village kama ishara ya kumpigania mtoto wa kike kupata elimu na kupinga ndoa za utotoni.

Akizungumza kituoni hapo jijini Arusha wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali, Mdee alisema pia ametoa vitu hivyo kama sehemu ya maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 ya Chadema.

Alisema watoto katika jamii wanafanyiwa ukatili mwingi, hivyo wanaojitokeza kulea watoto wanapaswa kupongezwa na kuungwa mkono kwani hilo ni taifa la kesho.

Hata hivyo, alisema akitokea mtu akapinga baadhi ya haki za watoto, lazima jamii isimame kuzitetea ili wapate haki yao.
Kama yeye anavyoshindwa kunyamaza anapoona baadhi ya mambo hayaendi sawa hata kama analala ndani.

Aliongeza kuwa katika maadhimisho ya jubilei wamepanga kufanya vitu mbalimbali kama shughuli za kijamii za kuwasaidia yatima na wazee.

Mdee alisema kinachomsikitisha ni kuona baadhi ya watu wanapambana kulea yatima, lakini hawapati fursa ya kusaidiwa na baadhi ya viongozi.

Naye Mratibu wa kituo cha Samaritan Village, Josephat Mmanyi, alimshukuru kwa msaada huo na kusema kituo kina watoto 50 wenye umri wa miaka 21 hadi mwaka mmoja na wapo ngazi mbalimbali za masomo,

Alitumia fursa hiyo kumwomba Mdee kupanda mti kituoni hapo ili kuamsha ari ya watoto wake wanaotamani kuwa wanasheria kama yeye kufikia azima hiyo.

Habari Kubwa