Mdee apokelewa kwa shagwe Bungeni, Ndugai aonya

11Nov 2019
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Mdee apokelewa kwa shagwe Bungeni, Ndugai aonya

MBUNGE wa Jimbo la Kawe ( Chadema),Halima Mdee leo amerejea bungeni kuendelea kushiriki vikao  baada ya kumaliza kutumikia adhabu aliyopewa ya kutoshiriki mikutano miwili tangu Aprili 2,mwaka huu kwa kosa la kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serili ( CAG) kwamba bunge ni dhaifu.

MBUNGE wa Jimbo la Kawe ( Chadema),Halima Mdee.

Aprili 2, mwaka huu Bunge liliazimia kuwa Mdee kutoshiriki mkutano wa Bajeti  wa 15 wa Bunge na mkutano wa 16 uliofanyika Septemba na Oktoba, 2019.

Mdee alitinga ndani ya mhimiri huo wa kutunga sheria majira ya saa tatu asubuhi wakati maswali na majibu na kuwasalimia baadhi ya wa wabunge wenzake huku akishangiliwa na wabunge wenzake wa upinzani.

Hali hiyo ilimlazimu, Spika wa bunge, Job Ndugai kuwaonya wabunge waliokuwa wanamshangalia Mdee.

" Mnaweza kumponza tena, nadhani mnanijua, nakuomba mheshimiwa Mdee ukae," amesema Spika Ndugai.

Baadaye Mdee alipata nafasi ya kuuliza swali kwa kutaka majibu ya serikali kuhusu fidia kwa wakazi wanaoishi eneo la Goba, Makongo juu wanaopisha ujenzi wa barabara inayoanzia Chuo Kikuu cha Ardhi-Makongo-Goba.

"Barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Makongo, Goba iko katika ujenzi baada ya kero ya muda, sasa naomba kujua fidia ya Sh.bilioni tatu kwa wakazi wa maeneo hayo waliopisha ujenzi watalipwa lini?," amesema Mdee.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaak Kamwelwe amesema suala la fidia lipo kwa mujibu wa sheria na siyo la makubaliano.

Habari Kubwa