Mdee, CCM wachafua hali ya hewa bungeni

25Apr 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mdee, CCM wachafua hali ya hewa bungeni

MJADALA wa makadirio ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka ujao wa fedha, jana uligeuka uwanja wa majibizano baina ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na Mbunge wa Siha (CCM), Dk. Godwin Mollel.

Majibizano hayo pia yalimlazimu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumtaka Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), kufuta kauli yake baada ya kusikika akimtukana tusi zito Mdee bungeni.

Chanzo cha malumbano hayo ni baada ya Mdee kudaiwa kulitumia vibaya jina la Rais wakati akizungumzia kuhusu mwenendo wa Kampuni ya Ndege (ATCL).

Majibizano makali yaliibuka wakati Dk. Mollel aliposimama na kuomba kumpa taarifa Mdee aliyekuwa anachangia mjadala huo bungeni mjini hapa jana mchana, lakini kabla Dk. Mollel hajapewa nafasi na Spika, Mbunge huyo wa Kawe alisikika akimwita mbunge mpya wa CCM huyo kuwa ni ‘Dk. Shika’.

“Nikiangalia randam ukurasa wa 11, mwaka huu wa fedha serikali inatarajia kufanya ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya ATCL, tutakumbuka mwaka jana serikali kupitia Waziri wa Fedha ilitenga Sh. bilioni zisizopungua 500 kwa ajili ya kununua ndege,” Mdee alisema.

“Hoja si kupinga ununuzi wa ndege. Hoja hapa ni fedha tunazowekeza ambazo ni matrilioni ya shilingi. Je, zinakwenda kuzalisha au tunakwenda kuzitupa na kupotea?

“Nina taarifa ya Msajili wa Hazina anasema ameshindwa kufanya uchambuzi wa kina wa utendaji kazi wa ATCL kutokana na kutokuwapo kwa taarifa za kutosha za kam- puni.

“Kwa mfano, hesabu za kampuni zilizoka- milika ni za mwaka 2014/15 tu yaliyofanywa na PWC ambayo hata hivyo mahesabu hayo hayajatazamwa wala kupitishwa na bodi. Hali hii inasababisha O si ya Msajili wa Hazina kushindwa kuchambua na kubainisha hali halisi ya uwekezaji ilivyo hadi sasa kuhusu madeni ya kampuni.

“Wanasema wanashindwa kujua hali ya ukwasi wa kampuni kwa sababu ya kampuni kutokuwa na mahesabu wa muda mrefu. Ukija kwenye taarifa ya ATCL wanasema shirika halikuwa na mpango wa biashara, yaani tunawekeza Sh. bilioni 500 na sasa tunawezeka Sh. bilioni 495 (mwaka 2018/19), hivi unawekezaje wakati hakuna mpango wa biashara?

“Msajili wa Hazina anasema shirika halina uzoefu wa kutosha. Bunge mwezi Januari walitoa taarifa za kamati na kuitwa wataalamu wa serikali wanaosimamia mashirika na

kusema shirika hili lina madeni ya Sh. bilioni 317. Sasa shirika lina madeni na kutokuwa na mpango wa biashara wala wataalamu tunaweka Sh. trilioni moja.

“Mimi niliombe Bunge tutekeleze wajibu wetu, hivi inaingia akilini kwamba kwenye kilimo kinachoajiri asilimia zaidi ya 75 ya watanzania tumeweka Sh. bilioni 100, lakini kwenye ndege tunakojua fedha tunaitupa chini tumeweka Sh. trilioni moja?

“Msije mkajiona mko salama hivi, fedha tukigundua mmeziwekeza kinyume na utaratibu kama nyaraka zinavyoonyesha tuta- wachukulia hatua. Ni muhimu Rais akajua hiyo kinga aliyonayo ya kikatiba inaangalia kama kuna mambo aliyofanya makusudi kwa kuona hakuna usalama mbele tutamshughulikia. Naongea kwa dhamira ya dhati, najua wabunge wengi wanajua.”

Maneno hayo ya Mdee kuhusu kinga ya Rais yalimwinua kitini Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Man- yanya, ambaye alieleza kuwa mbunge huyo wa upinzani alikiuka utaratibu katika kuchangia kwake.

“Ni kwamba, kwanza, (Mdee) achukulie kwamba Rais wa nchi ni kiongozi anayeheshimika na watu wote,” Manyanya alisema. 

“Pili, mambo yote yanayofanywa kwa nia njema yanatakiwa kuungwa mkono. Upinzani wenzetu wamekuwa wa kulalamika badala ya kutoa mawazo mbadala. Wabunge wa upinzani kipindi cha nyuma walikuwa wakichangia kuhusu ATCL na ndege zetu, wengine mmekuwa kama hamkumbuki. Siungi mkono michango ya kukashifu na wote kukashfu tunaweza.”

Baada ya Naibu Waziri huyo kuketi, Wa- ziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisimama na ali- poruhusiwa kuzungumza na Spika alisema: “Nilitaka nikuombe kuhusu utaratibu, nimsaidie Manyanya kwamba tunachokisema kuhusu Kanuni ya 64.”

“Kauni hiyo inasema hivi; ‘Mbunge yeyote akiwa anazungumza hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala au kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kuamua jambo lolote kwa namna fulani.” Lukuvi alisema jina la Rais halipaswi kutumika kwa namna alivyolitumia Mdee akieleza kuwa neno ‘kumshughulikia’ Rais kwa maoni yake halikuhusiana na mjadala huo.

Waziri huyo alimwomba Spika Ndugai kumtaka mbunge huyo aondoe maneno yake na kujielekeza katika mjadala ulikuwa mezani.

Hata hivyo, Mdee aliporuhusiwa kuendelea kuchangia, alisema Rais alichaguliwa na Watanzania, na Bunge ni la wawakilishi wa Watanzania, hivyo Rais lazima akosolewe na jina lake lazima litajwe kama anakwenda kinyume cha utaratibu.

“Ile dhana kuwa Rais haguswi lazima iishe. Bunge likiogopa kumtaja Rais wakati sisi tunapitisha bajeti na Rais ni sehemu ya Bunge, tunalifanyia makosa taifa hili. Sijatumia jina la Rais kwa kebehi. Nimesema tuna taarifa ya Msajili wa Hazina na ATCL zinazoeleza wazi... “ alise- ma Mdee lakini akakatishwa na Dk. Godwin Mollel aliyewasha kipaza sauti na kuomba kumpa taarifa mchangiaji.

Dk. Mollel ambaye hivi karibuni alijiuzulu nafasi ya ubunge wa Siha kupitia Chadema na kujiunga CCM kisha kutangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kupitia chama tawala, alidai kuna matatizo makubwa ya matumizi ya fedha ndani ya chama chake cha zamani (Chadema).

“Yeye (Mdee) kama kiongozi wa Chade- ma, katika chama chake asilimia 100 ya ma- pato hayaonekani, lakini leo kwenye chama hicho pasipo kuwapo na ruzuku na michan- go ya wabunge, chama hakiendesheki na miaka mingi hawana hata ‘investment’ (uwekezaji) yoyote,” Dk. Mollel alisema.

“Mheshimiwa Spika; kwanza nirekebishe. Wananiita Dk. Shika na nitawashika vibaya. Kwa maana hiyo...” (Spika Ndugai akawa- sha kipaza sauti na kusema ‘Mollel hatujakusikia vizuri anza tena’).

“Ninachosema Chadema hawana hata kibanda kwa ajili ya kupata kipato. Hata kama mnaweza kuwa na mawazo mazuri kwa miaka yote mmefanya nini Chadema ili tuamini mkichukua nchi mnaweza kufanya kitu?” Dk. Mollel alihoji.

Baada ya kupewa nafasi ya kuendelea kuhangia na kuulizwa na Spika kama anapokea taarifa ya Dk. Mollel, Mdee alisema: “Siwezi kumjibu Dk. Shika, bidhaa ya kichina hata mara moja. Nikimjibu nitakuwa najidhalilisha. Hoja yangu iko wazi kabisa”.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Mdee ilimwinua kitini Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma ambaye baada ya kuruhusu kutoa taarifa alisema: “Dk. Mollel alikuwa akitoa taarifa halali, 

kuna lugha inatoka inasema Dk. Shika na Mdee amesema Dk. Shika, jina hili linaingia katika dhihaka ya kumdhihaki mbunge.”

Wakati Musukuma akieleza hayo, Mbunge wa Mtera (Lusinde) alisikika akimtukana tusi zito Mdee na baada ya Spika kumruhu- su Waziri Kivuli huyo wa Fedha na Mipango kuendelea kuchangia, alisema:

“Mwenyekiti (Spika) nimetukanwa, Lusinde amenitukana tusi zito sana, sasa kama hajafuta na mimi nitatoa la kwangu kama hatofuta.”

Kutokana na kauli hiyo ya Mdee, Lusinde aliwasha kipaza sauti na kutangaza kufuta maneno aliyoyatamka dhidi ya mbunge mwenzake huyo.

“Nimefuta mwenyekiti,” alisema kwa kifupi Mbunge huyo wa chama tawala huku kukiwa na minong’ono ya wabunge ndani ya Ukumbi wa Bunge.

Kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai aliwataka watunga sheria wenzake kutulia akisema: “Anayesema ni Mdee, mwacheni aseme.” 

Habari Kubwa