Mdee, wenzake wafutiwa kesi Kisutu

05May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mdee, wenzake wafutiwa kesi Kisutu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifuta kesi ya wafuasi 27 wa Chadema akiwemo Halima Mdee na wabunge wengine wawili waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko na kutotii amri halali katika geti la gereza la Segerea jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo na kuachiwa huru leo Jumatano Mei 5, 2021 na mahakama hiyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri hilo.

Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.

Hakimu Shaidi ameifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi kwa muda mrefu. Miongoni mwa washtakiwa katika kesi hiyo ni mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na wabunge wenzake, Ester Bulaya na Esther Matiko.

Mbali na wabunge hao, washtakiwa wengine ni, aliyekuwa meya wa manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob; Patrick Assenga; mfanyabiashara, Henry Kilewo na wengine 21.

Kabla ya kufutwa kwa kesi hiyo, wakili wa Serikali mwandamizi, Mkunde Mshanga amedai kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi lakini upande wa mashtaka hawakuwa na shahidi na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutotii amri halali iliyotolewa na askari Magereza tukio wanalidaiwa kutenda Machi 13, 2020 eneo la gereza la Segerea lililopo wilaya ya Ilala.

Siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa makusudi walikaidi amri halali ya kuondoka eneo la gereza kwa amani ili eneo hilo libaki wazi, amri hiyo iliyotolewa na askari mwenye namba B 3648 sajenti John ambaye ni mlinzi wa geti la gereza hilo.

Habari Kubwa