Mdude wa Chadema aweka msimamo

21May 2019
Romana Mallya
DAR
Nipashe
Mdude wa Chadema aweka msimamo

MWANAHARAKATI Mdude Nyangali maarufu (Mdude Chadema), amefunguka na kueleza kuwa licha ya kutekwa na watu wasiojulikana na kupigwa kipigo ambacho hajawahi kukipata, hataacha harakati zake mitandaoni.

MWANAHARAKATI Mdude Nyangali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mdude alisema tukio lililomtokea Mei 4, mwaka huu, ni la utekaji na si kwamba alipotea kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alivyoeleza bungeni.

Alisema anamtilia shaka Masauni kuwa anawajua waliomteka na kumwomba Rais John Magufuli amfute kazi.

"Kuna uhusiano kati ya maelezo ya Masauni bungeni aliyowataka vijana wawe makini kwenye mitandao kwa kuichafua serikali kuwa hawatawavumilia na wakati nimetekwa watekaji waliniambia kuwa nimeichafua serikali ninatumiwa na mabeberu," alisema.

Alisema kwa kauli hizo mbili, anamtuhumu Naibu Waziri Masauni kuwa anawajua watekaji.

Pia alilituhumu Jeshi la Polisi kuwa ndilo lililohusika na tukio la kutekwa kwake kwa sababu licha ya kutokea mita chache kutoka kituo cha polisi kilipo na yeye kupiga kelele za msaada, hakusaidiwa.

"Mwizi hawezi kujichunguza. Ninachotaka ni uchunguzi huru, tunaweza kuita shirika lolote lililobobea kwenye uchunguzi lije kuchunguza tukio hili," alisema.

Wakati akisimulia tukio hilo, mwanaharakati huyo alijikuta akilia na kueleza kuwa alitekwa na kundi la watu waliokuwa kati ya wanane na tisa wakiwa na silaha na magari wawili aina ya Land Cruiser na Nissan Patrol, moja likiwa halina namba na walimpiga hasa kichwani.

Alisema watekaji hao walimpiga kipigo ambacho hakuwahi kupigwa licha ya matukio kadhaa kumkuta awali.

Mdude alidai kuwa tukio hilo ni la utekaji kwa sababu eneo alilochukuliwa ni mwenyeji na ameishi hapo zaidi ya miaka 20 hata akitembea akiwa amefumba macho anajua anakokwenda.

"Kutekwa kwangu kunahusiana na masuala ya siasa kwa sababu ya itikadi yangu. Mimi  ni Chadema na ni kiongozi wa kanda, mimi ni Ofisa Mafunzo na Oganizesheni Kanda ya Nyasa ambayo ina mikoa mitano na Mwenyekiti wa Kanda ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Katibu wa Kanda ni Emmanuel Masonga," alisema.

Mdude alibainisha kuwa jambo ambalo limesababisha atekwe ni kutokana na misimamo yake ambayo imekuwa ikilenga kukosoa mambo mbalimbali.

"Kwa kuwathibitishia zaidi kwamba tukio langu ni la kisiasa ni maneno ya watekaji. Ilikuwa tarehe 4 (Jumamosi), siku moja baada ya Rais John Magufuli kumaliza ziara mkoa wa Mbeya. Kwangu ilikuwa siku ya kwanza kuonekana hadharani kwa sababu sikuwapo muda, nilitembelea ofisini kwangu asubuhi," alisema.

Kuhusu kubadili msimamo wa kisiasa alisema: "Kazi ya sikio haiwezi kufanywa na pua, pua itafanya kazi yake na sikio kazi yake. Siwezi kubadili msimamo wangu na mkae mkijua ujasiri ni asili ya mtu," alisema.

"Nimezaliwa hivi hivi kama kuna maiti au umauti unanitafuta ni mara mia kwenye maisha, ni bora kifo huwa kina tisha sana lakini kifo ni kizuri kama unakufa ukiwa unawapigania wanyonge na watu ambao hawawezi kusema, kifo ni kibaya kama unakufa unawadhulumu wanyonge," aliongeza.

Mdude aliwashukuru viongozi wa dini waliofanya kazi ya kupiga kelele baada ya tukio hilo na kuwaomba waendeleze kwa wengine ambao hawajapatikana hadi sasa.

Habari Kubwa