Membe achukua NEC kusaka urais

08Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Membe achukua NEC kusaka urais
  • *Asema hatakuwa rais wa wanyonge tu, bali Watanzania wote

MGOMBEA urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe, amechukua fomu kwenye Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo, akiahidi hatakuwa rais wa wanyonge tu, bali wa Watanzania wote.

Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifika jana kwenye Ofisi za NEC akiwa amefuatana na Mgombea Mwenza wake, Profesa Omary Fakiy Hamadi, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu, Ado Shaibu na viongozi wengine wa chama.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Membe alisema: "Mimi sitakuwa rais wa wanyonge tu, nitakuwa rais wa Watanzania wote, ili kuisaidia nchi kukua kiuchumi, iendelee na dunia ifaidi.”

Membe aliendelea kusisitiza kaulimbiu ya 'Yajayo Yanafurahisha’, akibainisha kuwa kilichomsukuma kugombea nafasi hiyo ni kukereketwa na dhamira yake ya kutatua matatizo ya wananchi.

Alisema Watanzania wanasubiri kwa hamu kupata Rais atakayetatua matatizo yao katika kipindi chake cha urais.

“Na mimi ni miongoni mwa watu ambao ninataka kusema wazi kabisa kilichonisukuma kugombea urais wa Tanzania ni kukereketwa kwangu na dhamira yangu ya kutatua matatizo ya wananchi. Mimi sitakuwa rais wa wanyonge tu, nitakuwa rais wa Watanzania wote," alisema.

Mgombea huyo aliahidi kuwa ACT -Wazalendo itaendesha kampeni zake kistaarabu kwa kutoa hoja za kuwashawishi wananchi waichague.

“Uchaguzi huu tutaendesha kwa ustaarabu mzuri sana na tutakuwa wastaarabu sana, tutakuwa tunakwenda na hoja za kuwashawishi Watanzania waichague ACT-Wazalendo kuchukua awamu hii ya uongozi kutoka kwa Mzee wetu John Magufuli kuileta kwa Mzee Membe ili tuweke mambo sawa.

“Hatutatukana mtu, tutaheshimu, tutakuwa tunapambana kwa hoja, kutambua kero za wananchi na namna ya kuzitatua. Ninaomba waandishi wa habari wote, hiki ni kipindi cha kusimama na kuwaeleza Watanzania msipendelee mtu mmoja, mtafanya dhambi kubwa. 'Yajayo yanafurahisha sana'," alisema.

Membe alisema mchakato wa kuwatafuta wadhamini 200 katika mikoa 10 nchini utaanza leo na kuwahakikishia Watanzania kuwa ana afya njema.

“Nitatimba nchi nzima, mikoa yote kutafuta wadhamini na wapo wengi, na kivumbi kitakapoanza rasmi tarehe 26, nitawafikia Watanzania wote popote nitakapokwenda, ningependa kusema jambo moja, uchaguzi huu ni wakipekee sana," alisema.

Akitoa maelezo kabla ya Membe kukabidhiwa fomu, Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera, alisema fomu namba 8A inatumika kwa ajili ya uteuzi wa wagombea kiti cha rais na makamu wa rais ambayo imeandaliwa na tume.

“Mtawapatia seti nne ya fomu namba 8A ambayo ni fomu ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha urais na makamu wa rais na kila seti kutakuwa na nakala 10 za fomu hizo, ili kuwawezesha kujaza idadi ya wadhamini inayotakiwa,” alisema.

Alibainisha kuwa watatakiwa kudhaminiwa na wapigakura wasiopungua 200 ambao wamejiandikisha kupiga kura katika kila mkoa kwenye mikoa 10 na kati ya hiyo, angalau miwili kutoka Zanzibar.

“Majina ya wadhamini katika seti zote yanatakiwa kufanana, pia mtapaswa kuwasilisha fomu za uteuzi kwa wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo kule ambako mtaenda kutafuta wadhamini ili watoe uthibitisho kwa wadhamini hao. Tume imeshawapatia wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo yote nakala tepe na orodha ya wapigakura wa majimbo yote ili waitumie kwa kazi hiyo,” alisema.

“Kutakuwa pia na tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi kwa ajili ya rais, ambapo mtapatiwa fomu namba 10, pia kutakuwa na nakala nne kwa ajili ya mgombea wa kiti cha rais na nne kwa mgombea wa kiti cha makamu wa rais."

Akikabidhi fomu, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage, pia alisema katika mkoba wa fomu, kuna nakala nane za fomu namba 10 ya tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.

“Ninawapongeza kwa kutumia haki yenu ya kuchagua na kuchaguliwa ya kikatiba na ushiriki wenu utachangia kudumisha demokrasia nchini mwetu," alisema.

Habari Kubwa