Membe akoleza moto tume huru ya uchaguzi

20Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Membe akoleza moto tume huru ya uchaguzi

ALIYEKUWA kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Membe, amesema tume huru ya uchaguzi haikwepeki ili kuwa na uchaguzi huru na haki.

ALIYEKUWA kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Membe, picha mtandao

Kwa mujibu wa taarifa aliyoandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, alisema jambo hilo alilizungumza hata alipoitwa na kamati ya maadili ya kilichokuwa chama chake kwa ajili ya kuhojiwa Februari, mwaka huu.

“Nilisema hili kwenye kamati ya maadili na ninasema tena. Kwa mazingira ya kisiasa yaliyopo tunahitaji tume ya uchaguzi ambayo ni huru, yenye uwakilishi na uwazi kwa ngazi ya taifa na wilaya. Ninaunga mkono kwa nguvu zote sauti zote za kudai hili,” alisema.

Februari 28, mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM ilitangaza kumfukuza Membe ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika serikali ya awamu ya nne na Mbunge wa Mtama kwa miaka 15, kwa kile kilicholeezwa ni kwenda kinyume cha matakwa ya chama hicho.

Wakati Membe akivuliwa uanachama, Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, alipewa karipio na kutakiwa kutogombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho kwa miezi 18, huku Katibu Mkuu mwingine mstaafu, Yusuph Makamba, akiomba msamaha na hatimaye kusamehewa.

Kwa muda mrefu vyama vya upinzani vimeendelea kudai tume huru ya uchaguzi kwa madai kuwa iliyopo sasa haiwatendei haki kutokana na muundo wake.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama hicho kitaanza mikutano ya hadhara ya kudai tume huru ya uchaguzi kwa kuwa iliyopo kimuundo haiwatendei haki kwa kuwa watendaji wake ni wateuliwa wa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.

Februari mwaka huu, Mbowe akiwa kwenye mziba wa Elias Mwingira, baba wa kiongozi wa kanisa la Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira, alisema ni lazima kuwa na tume huru kabla ya uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.

Pia Januari 29, mwaka huu, alisema amemwandikia Rais akiomba serikali kufanya mabadiliko ya sheria yatakayowezesha kuunda kwa tume huru kabla ya Oktoba.

Naye Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alikaririwa mara kadhaa akisema kuwa tatizo si uchaguzi kufanyika bali ni tume huru ambayo itatenda haki kwa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.

Zitto akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama hicho, alisema msimamo wa chama hicho katika chaguzi zijazo ni kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi, ili uchaguzi wa Oktoba usiwe na dosari kama zilizojitokeza kwenye uchaguzi uliopita.

Kiongozi huyo alikwenda mbali zaidi na kuvitaka vyama vyote kuungana kudai tume hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema chama hicho kinahitaji katiba mpya ili uchaguzi mkuu wa Oktoba uwe huru na haki lazima kuwe na tume huru.

Machi mwaka huu, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia, alisema tangu kuasisiwa kwa chama hicho mwaka 1991 hitaji limekuwa katiba mpya ambayo ndani yake itakuwa na tume huru ya uchaguzi.

Hata hivyo, Machi 6, mwaka huu, Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally, alipotembea vyombo vya habari vya IPP, alisema tume hiyo iko huru na kwamba uchaguzi utakuwa huru, haki na salama.

“Nawahakikishia Serikali za CCM zina dhamana ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira huru, haki na salama,” alisema.

“Rais Magufuli amekusanya kodi, nawahakikishia tume itapata fedha za kutosha…kwa mara ya kwanza tutaendesha uchaguzi bila kutumia fedha za wafadhili, hiyo nayo ni uhuru, tume tegemezi haiwezi ikaendesha uchaguzi huru, unaweza kuona huru kwa macho lakini kuna mtu kaleta fedha, anakuleta tekonolojia ikiziba unaletewa mtaalamu kuzibua,” alisema.

“Wakati wanafanya vizibo yeye ndiyo anajua kizibo gani kimewekwa na akichelewa mnatafutana manakaa siku saba hamjapata matokeo…uhuru wa uchaguzi ni pamoja na nchi kugharamia uchaguzi wake wenyewe na kutumia wananchi wake kusimamia uchaguzi,” alisisitiza.

“Mahitaji ya tume huru ni zaidi ya tume yenyewe, mahitaji ya uchaguzi huru na haki ni zaidi ya kazi zitakazofanywa na tume, tunanze kujiandaa kujenga imani katika tume, polisi, vyama vya siasa na wapiga kura,”alisema.

Januari mwaka huu, Rais John Magufuli alipokutana na mabalozi wa nchi zenye balozi nchini, aliwahakikishia kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru, amani na haki.

Pia Ubalozi wa Marekani nchini, ulitoa taarifa ukitaka kuharakishwa kwa uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa wanaoaminika watakaofuatilia uchaguzi kwa kipindi kirefu na kifupi.

Habari Kubwa