Membe anawa mikono CCM

07Jul 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Membe anawa mikono CCM

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa utawala wa awamu ya nne, Bernard Membe, amerejesha kadi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Membe (66), alikabidhi kadi hiyo jana katika Kijiji cha Rondo mkoani Lindi, akisindikizwa na mke wake pamoja na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho.

"Nimemwandikia Katibu Mkuu wa CCM (Dk. Bashiru Ally) kuhusu tukio hili na kukishukuru chama kwa mema kilichonitendea. Ninawatakia kila la heri viongozi na wanachama wote," Membe aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter muda mfupi baada ya kukabidhi kadi hiyo.

Juzi, Membe alizungumza na mwandishi mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, akiahidi kurudisha kadi hiyo kama ishara ya kujitoa rasmi kwenye chama hicho tawala.

Alisema amefukuzwa na chama chake kwa madai ya utovu wa nidhamu, hivyo itakapofika Julai sita (jana) Jumatatu, atarejesha kadi kwa wenyewe, ili wajue kwamba ameshajitoa rasmi.

“Ni kweli nilifukuzwa kwenye chama changu na ninaomba nitumie fursa hii kuutangazia umma kuwa siku ya Jumatatu Julai 6 nitarejesha rasmi kadi ya CCM kwa wenyewe,” Membe alisema wakati akijibu swali aliloulizwa na Ulimwengu.

Februari 28 mwaka huu, CCM ilitangaza kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imemvua uanachama Membe baada ya kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho.

Kamati hiyo inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Phillip Mangula, ilimhoji Membe kwa saa tano kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho mkoani Dodoma Februari 6 mwaka huu.

Mbali na Membe, makada wengine wa CCM waliohojiwa kwa nyakati tofauti ni makatibu wakuu wastaafu, Abdulahman Kinana na Yusuf Makamba, ambao chama kiliwapa onyo na kuwasamehe baada ya kuomba msamaha.

Baada ya kutoka kuhojiwa, Membe alisema safari ya kwenda Dodoma ilikuwa na manufaa makubwa kwake, kwa chama na kwa taifa zima.

Habari Kubwa