Membe, Maalim Seif wapita kuwania urais

06Aug 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Membe, Maalim Seif wapita kuwania urais

MKUTANO Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, umewapitisha Bernard Membe na Maalim Seif kuwa wagombea wa urais wa Tanzania na Zanzibar, mtawalia, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu.

Mgombea urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe (wa pili kushoto), akisalimiana na mgombea urais wa CHADEMA, Tundu Lissu, wakati wa Mkutano Mkuu wa ACT, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: ANTHOMY SIAME

Wagombea hao walipitishwa jana katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Katika hotuba yake, Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alisema endapo watapewa fursa ya kushika dola, serikali watakayoiunda itahakikisha kila Mtanzania ana kuwa na haki ya kufurahia utanzania wake kulingana na kaulimbiu yao ya ‘Kazi Na Bata’.

Alisema wanataka Watanzania wafanye kazi kwa bidii na pia wafaidi matunda ya jasho lao na wawe na raha na furaha.

“Tunataka serikali zitakazoongozwa na ACT-Wazalendo, zikatae kuona vijana wa Tanzania Bara na visiwani Zanzibar wananyang’anywa fursa, wanakatishwa ndoto zao, wanakandamizwa na kufanywa watwana ndani ya taifa lao,” alisema.

Zitto alisema wataandaa maisha stahiki ya uzeeni kwa kuwa na mfumo madhubuti wa hifadhi ya jamii kwa wote na kila mtu kuwa na uhakika wa bima ya afya na pensheni.

“Tuwe na elimu bora yenye kukidhi vigezo vya soko la ajira na kuwaandaa wahitimu kuvumbua na kujiajiri. Vijana wote watakaojiunga na elimu ya ufundi, watasoma bila malipo ili kuondoa kikwazo cha vijana kupata stadi na ujuzi kuendesha maisha yao,” alisema.

Zitto aliongeza kuwa watahakikisha uchumi wa taifa litakaloongozwa na chama hicho utakuwa jumuishi na endelevu.

“Tunataka serikali ambayo itaboresha na kuwezesha ustawi wa sekta isiyo rasmi hasa ya biashara ndogo ambazo nyingi zinafanywa na wanawake na vijana,” alisema.

Zitto aliendelea kusema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wa kuchagua uhuru wa kweli kwa kila mtu na kuwa na maendeleo jumuishi ya watu dhidi ya maendeleo ya vitu.

Kabla ya kupitishwa, Maalim Seif aliwataka wanachama wafanye uamuzi wa hekima na busara kwa kuwachagua wagombea wazuri ambao watakwenda kuleta ushindani kwa vyama vingine.

Alisema Watanzania wanataka mabadiliko, hivyo ni lazima wapate wagombea wazuri watakaounda serikali itakayotekeleza yaliyoahidiwa na vyama.

Alisema mgombea yeyote atakayeshinda kwa uhalali Zanzibar, atampa mkono na kumpongeza na kutoa angalizo kuwa ACT-Wazalendo wakishinda, kusifanyike mbinu ya kuwanyang'anya ushindi.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema msisitizo wao kwa vyama ni kuheshimu sheria za nchi za vyama kuelekea uchaguzi huo.

“Uchaguzi ni ushindani, tunaelewa siasa za ushindani kuna mbwembwe nyingi. Mwenyekiti wa chama (Maalim Seif) amesema mtalinda ushindi, sisi tunasema mlinde kwa mujibu wa sheria, fanyeni mbwembwe zote za kisiasa, ila kwa mujibu wa sheria,” aliagiza.

Mgombea urais kupitia CHADEMA, Lissu alisema mwaliko alioupata aliutegemea kwa sababu ACT-Wazalendo ni marafiki wa kweli na kwamba hata wasingemwalika angekwenda mwenyewe.

“Akufaaye wakati wa dhiki ndiye rafiki, kwa sababu kuna kipindi binafsi nilikuwa kwenye dhiki na nililala siku kadhaa, nilipoamka nikakuta nipo kwenye nchi nyingine, mazingira tofauti.

“Katika watu waliokuja kuniangalia miongoni ni Maalim Seif na wengine walinifuata Brussels Ubelgiji, Zitto alikuja zaidi ya mara moja na familia yake, Fatma Karume alikuja, alikuwa ananililia, nipo kitandani nikamwambia yatakwisha," Lissu alisema.

Alikiahidi chama hicho kuwa ushirikiano unaozungumzwa wataufanya ila kwa kuangalia kama maeneo watakayoshirikiana ni ndoano au salama.

*Imeandaliwa na Romana Mallya, Mary Mshami, Fatma Mtutuma na Magdalena Haule.

Habari Kubwa